Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango Halmashauri ya Wilaya ya Meru wamefanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo.
Kati ya miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ukamilishaji wa vyumba 2 vya madarasa shule ya Sekondari ya King'ori iliyopo Kata ya Malula ambayo ilipatiwa fedha kutoka Serikali Kuu kwa mpango wa kuboresha Elimu ya Sekondari ( SEQUIP) kiasi cha shilingi Milioni 25 .
Aidha, Wajumbe wamekagua umaliziaji wa jengo la Zahanati ya Ngejisosia iliyopo Kata ya Malula iliyopelekewa fedha kutoka mapato ya Ndani kiasi cha shilingi Milioni 32.
Miradi mingine iliyokaguli ni ukamilishaji wa madarasa mawili katika shule ya Sekondari Kitefu na Ukarabati wa Madarasa Mawili Shule ya Msingi Nkoanekoli.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Jeremia Kishili ametoa pongezi wa Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu wa shule hizo pamoja na Zahanati kwa usimamizi mzuri wa matumizi ya fedha katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Vilevile, amesisitiza walimu kuhakikisha wanawachukulia hatua wazazi na walezi ambao hawachangii Chakula shuleni, kwani kutofanya hivyo ni kurudisha nyuma maendeleo ya taaluma ya mtoto awapo shuleni.
" Serikali imetoa fedha nyingi kuhakikisha wanafunzi wanakuwa katika mazingira bora ya kusomea, lakini tukumbuke kuwa mtoto hawezi kusoma au kumsikiliza mwalimu akiwa na njaa. Hivyo kwa wale wazazi watakaokaidi kuchangia chakula shuleni hatua zichukuliwe ili waweze kuchangia" amesema Mhe. Kishili.
Katika hatua nyingine Wajumbe hao na timu ya Menejimenti wametoa pongezi na kuchangia zaidi ya fedha sh. Laki 2 na nusu kwa Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Nkoanekoli kwa usimamizi mzuri wa fedha shilingi Milioni 7 walizopokea kutoka mapato ya Ndani ya Halmashauri kwa ajili ya ukarabati wa madarasa mawili.
Mwenyekiti wa Halmashauri kwa niaba ya wajumbe wote amemkabidhi mwalimu mkuu fedha hizo kama mchango wa kuanzia kununua mifuko ya simenti ya kufanya ukarabati wa darasa jingine na kuahidi kutafuta fedha za kuwaongezea ili kukarabati madarasa mengine kwani shule hiyo ni kati ya shule kongwe iliyoanzishwa mwaka 1963.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa