Vijana waliohitimu kozi kwa mujibu wa Sheria Operesheni miaka 60 ya Jeshi la kujenga Taifa 2023 Kikosi 833 wametoa mapendekezo ya kuongezewa muda wa miezi 6 ya mafunzo hayo.
Mapendekezo hayo yametolewa Leo kwa Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika kambi ya Oljoro Wilayani Arumeru.
"Service Girl" Anna T. Minja kutoka Kilimanjaro ameeleza kuwa mbali na kujifunza masuala ya ukakamavu kwa kipindi cha miezi mitatu wameweza kujifunza kilimo na ujasiriamali ili iweze kuwasaidia watakapokuwa uraiani.
"Tumejifunza kulima bustani za mbogamboga kama mchicha, karoti na nyanya, lakini pia tumejifunza kutengeneza sabuni za maji, hii itatusaidia hata kwenda kujiariji." amesema service girl Anna.
Ameongeza kwa kusema kuwa wamejifunza namna ya kujikinga na adui,kulitumikia Taifa, kuwa na utii kwa wakubwa na wadogo lakini wamejifunza kuwa wazalendo. Zaidi amesema jeshi ni zuri linawajenga kiafya na kiakili.
Aidha, "Service man" Eliudi L. Lengidale kutoka Arusha ameeleza kuwa mafunzo kwa Mujibu wa Sheria yamewafanya kuwa wakakamavu na kuweza kufanya shughuli zozote za kijamii.
"Mafunzo haya yametusaidia kutujenga na kuweza kutatua changamoto zozote za maisha,lakini yametufanya kujitambua na kuepuka kujiingiza kwenye makundi ya vijana wasio na maadili" Amesema service man Eliudi.
Salama Abubakari ni Mzazi wa Haruna Abubakari ambaye naye amehitimu mafunzo kikosi 833, ameeleza kuwa ameshuhudia mabadiliko makubwa kwa kijana wake kabla ya kupata mafunzo na baada ya mafunzo.
"Kijana wangu amekuwa mkakamavu na nidhamu ya hali ya juu, nalishukuru jeshi la kijenga Taifa na Serikali kwa ajili ya watoto wetu, pia niwatoe wasiwasi wazazi wengine wasiogope kuwaleta watoto wao kujiunga na jeshi kabla ya kwenda vyuoni" amesema mzazi huyo.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Kaganda ambaye pia ni mgeni rasmi katika hafla hiyo, ametoa rai kwa vijana waliohitimu mafunzo hayo kuwa mafunzo waliyoyapata wakayatumie katika kuilinda na kuitetea nchi ya yetu ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kufuata Sheria zilizoweka na Nchi.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa