Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Arusha Ndg. Thomas Ole Sabaya ametoa utaratibu kwa Watendaji wa Kata katika Mkoa wa Arusha kuwasilisha taarifa za mapokezi ya fedha na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutoka katika Kata zao na kuziwasilisha katika vikao vya Kamati ya Siasa Mkoa, Wilaya, Kata na vikao vingine vya ngazi ya Vijiji na Vitongoji.
Utaratibu huo aliouanziasha ni maelekezo ambayo ameyatoa kwa lengo la kuhakiki wananchi kuanzia ngazi ya chini wanafahamu Serikali iliyopo madarakani inafanya nini kwa wananchi wake.
" Leo tutapokea taarifa kutoka katika Kata zote zilizopo Halmashauri ya Meru, Watendaji watatuambia wamepokea fedha shilingi ngapi kwenye Kata zao, lakini watatuambia utekelezaji wa fedha hizo na kama Je! taarifa hizo zimewasilishwa kwenye vikao vya ngazi zote za Kamati ya Siasa na vikao vingine vya kisheria? " amesema Sabaya .
Aidha, Sabaya ameeleza kuwa wananchi wakielewa Serikali yao inafanya nini wataongeza imani, lakini pia wananchi watajua kodi zao zinaenda kutekeleza miradi katika maeneo yao.
Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 Sura ya Kwanza Ibara ya 10 na 11 imeeleza kuwa, "Chama hicho kitahakikisha Serikali zake zinatekeleza mambo yote yaliyoahidiwa Katika Ilani hiyo na kwa manufaa na ustawi wa Taifa ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto za wananchi.