Wananchi wa Kata ya Mbuguni, Shambarai Burka, Majengo, Makiba na Maroroni wamepatiwa elimu ya tahadhari ya majanga ya Mvua kubwa za El Nino zinazoweza kutokea kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini.
Timu ya Afya moja ya kukabiliana na Majanga(One Health) kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Meru ikiongozwa na Mwakilishi wa Mratibu wa Maafa Bi. Digna Massawe (Afisa Kilimo) wamefika katika Kata ya Majengo, Mbuguni, Shambarai Burka, Makiba na Maroroni na kutoa elimu ya kukabiliana na tahadhari ya Mvua kubwa za El Nino katika maeneo yao.
Kati ya tahadhari zilizotolewa ni pamoja na Kuepuka kutembea sehemu hatarishi kwenye mikondo ya Maji, Mabwawa au kukatiza kwenye maji yaliyofurika kwenye barabara, kuhama sehemu za mabondeni, kufukua mitaro ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi.
Askari wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji CPL . Beda Marwa ametoa elimu ya kukabiliana na tahadhari hizo na kuongezea kwa wenye vyombo ya moto kuendesha magari kwa mwendo wa wastani kipindi cha mvua kwani kuna kuwa na uoni hafifu unaoweza kusababisha Majanga. Pia, ameomba ushirikiano kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la zima moto na uokoaji kwa kupiga namba 114.
Afisa Kilimo, Bi. Digna Massawe ameeleza kuwa kipindi hichi cha mvua ni kipindi kizuri cha kuotesha mazao ya muda mfupi kama Mahindi, maharage na mazao mengine ya nafaka, mbogamboga na matunda.
Afisa Mifugo Dkt.Charles Msigwa amesisitiza kuchanja Mifugo kwa kipindi hichi cha mvua ili kuepukana na magonjwa kama Kimeta, bacteria, Kupe, minyoo, Protozoa na magonjwa mengine. Pia, amesisitiza kuogesha Mifugo kila baada ya siku 14 na kuwapa mifugo dawa za Minyoo kila baada ya miezi mitatu.
Afisa Afya Petro Mchelo ametoa elimu ya kukabiliana na tahadhari kwa kufunika vyoo ili mvua zinaponyesha mafuriko yasichukue uchafu na kusambaza katika maeneo na kusababisha magonjwa ya mlipuko kama kuhara, kuumwa matumbo na kipindupindu. Pia amesisitiza kunywa maji safi na salama ambayo yamechemshwa.
Hata Hivyo, Afisa Mazingira Naima Temba ametoa elimu ya Kukabiliana na tahadhari hiyo kwa kuhifadhi taka vizuri ili kuzuia mlipuko wa magonjwa, kuzuia watu kupita kwenye kingo za mito kwa kuwa kuna mmomonyoko wa udongo lakini kuzuia watoto wasicheze kwenye madimbwi au maji yaliyotuama. Pia amesisitiza kuweka miundombinu ya kuvuna maji ya Mvua.
Vilevile, Afisa Maliasili Consolatha Mtuy ametoa elimu ya kukabiliana na tahadhari ya kutojificha chini ya miti kwa lengo la kujikinga na mvua. Aidha, ameeleza kuwa, kama kuna miti imeonekana kuwa na hatari ya kuanguka taratibu zifuatwe kwa kuomba kibali cha kukata mti huo ili kuebuka madhara yatakayojitokeza. Pia amesisitiza zoezi la kuotesha miti kipindi cha mvua. Kwa kutazama video zaidi bofya
https://www.youtube.com/watch?v=3pxFscArKaQ
https://www.youtube.com/watch?v=-nFF-QMnsx8
https://www.youtube.com/watch?v=jDJFjAKB98Q
https://www.youtube.com/watch?v=G-owaEqbNoc
https://www.youtube.com/watch?v=fM8IzXsZ5CI
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa