Shamba lililokuwa Mali ya Arusha Corparative Union (ACU) ambalo ni namba 59, lililokuwa na ekari 309 lililopo kitongoji cha USA Madukani limetolewa kwa wananchi waliokuwa tayari wamefanya makazi katika maeneo hayo kwenye zaidi ya ekari 242.6.
Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Kaganda aliwataka wataalamu kutoka Halmashauri ya Meru kuwashauri ACU pamoja kutafuta hatua nzuri za kuondoa mgogoro katika eneo hilo na ndipo tarehe 7 Machi 2024, ACU waliomba ofisi ya Mkurugenzi kumega eneo ambalo wananchi wamevamia na wao kubakia na eneo ambalo halijavamiwa.
Aidha, baada ya hatua hiyo Mhe. Kaganda ametoa maelekezo kwa wananchi hao ikiwa ni pamoja na kupata hati Miliki ya Maeneo hayo kutoka kwa wataalamu na kuhakikisha pia maeneo hayo yanapimwa lakini pia ameendelea kuwataka wananchi wa Wilaya ya Arumeru kutokutumia Fursa hiyo kuendelea kuvamia maeneo ya Wawekezaji kwani sheria itafuata Mkondo wake.
Kwa upande wake Afisa ardhi wa Halmashauri ya Meru Bw. Leonard Mpanju ametolea ufafanuzi kwa wananchi hao kufuatia utaratibu wa upimaji wa maeneo hayo utakaofanyika hivi karibuni ikiwa ni pamoja na gharama za uchangiaji katika ulipaji wa kodi na upatikanaji wa hati.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa