Wajumbe wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Meru, wamepitisha Mpango na Bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kwa makadirio ya mapato na matumizi ya kiasi cha shilingi bilioni 47,366,414,216.08 na kuelekeza Halmashauri kuzingatia vipaumbele vitakavyowaletea wananchi maendeleo wakati wa utekelezaji wa bajeti hiyo.
Akiwasilisha Mpango na Bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo Ndg. Maarufu Mkwaya ameeleza kuwa mwaka wa fedha 2020/2021, Halmashauri hiyo imepanga kukusanya, kupokea na kutumia kiasi cha shilingi 47,366,414,216.08 ambapo Shilingi Bilioni 3.4 ni fedha za Mapato ya Ndani ya Halmashauri hiyo na jumla ya Shilingi Bilioni 43 ni fedha za ruzuku toka Serikali Kuu zinazojumuisha Mishahara, Matumizi Mengineyo na fedha za miradi ya Maendeleo.
Aidha, Mkwaya amefafanua katika Bajeti hiyo ya mwaka wa fedha 2020/2021, fedha za Miradi ya Maendeleo kutoka mapato ya ndani ni shilingi Milioni 660 sawa na 40% ya mapato ya ndani yanayotarajiwa kukusanywa. Aidha, bajeti ya miradi ya maendeleo kwa fedha toka Serikali Kuu ni shilingi Bilioni 6.9.
Kwa upande mwingine, Halmashauri imetenga jumla ya Shilingi 165,162,296.51 kwa ajili ya utoaji wa mikopo ya kiuchumi kwa vikundi vya Wanawake Vijana na Watu wenye ulemavu.
Diwani wa Kata ya Kikwe Mhe. Paulo Shango amesema ili kuweza kukusanya mapato na kuwaleta wananchi maendeleo Halmashauri haina budi kubuni vyanzo vipya vya mapato sambamba na kuboresha vilivyopo ikiwemo kuongeza idadi ya meza za chuma katika soko la Tengeru na masoko mengine ambazo zitakodishwa kwa Wafanyabiashara.
Aidha, wajumbe walitoa wito kwa Meneja wa Halmashauri wa Wakala wa barabara Mjini na Vijijini (TARURA) kufanya kazi kwa karibu na Halmashauri na kuhakikisha anatoa taarifa sahihi ili wananchi wawe na uelewa wa mipango na utekelezaji wa matengenezo ya barabara na kuondoa sintofahamu kwa wananchi wakati wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara.
Akitoa ufafanuzi kwa Waheshimiwa Wajumbe, Meneja wa TARURA Halmashauri ya Meru Mhandisi Lawrance Msemo amepokea ushauri na kueleza kuwa changamoto kubwa ni bajeti ikilinganishwa na uhitaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ndg. Emmanuel Mkongo ameeleza kuwa Halmashauri ipo tayari kushirikiana na TARURA katika matengenezo ya barabara za Halmashauri kwa kutumia fursa ya mitambo ya Halmashauri , kwani kwa kufanya hivyo kutachochea shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri hivyo kukuza kipato cha wananchi.
Akihitimisha Mkutano huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mheshimiwa Willy Njau alisisitiza ushirikiano wa kutosha kati ya Waheshimiwa Madiwani na wataalam ili kufikia malengo na vipaumbele vilivyowekwa.
Ikumbukwe kuwa Mkutano huo umefanyika kwa siku mbili ambapo siku ya kwanza ulipitia utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha uliopita 2018/2019 ya Bilion 45.8 sambamba na utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu 2019/2020 kwa kipindi cha miezi 6 Julai hadi Disemba 2019 Shilingi Bilion 43.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mhe. Willy Njau akizungumza wakati wa baraza la Halmashauri hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Ndg. Emmanuel Mkongo akizungumza wakati wa baraza la Halmashauri hiyo.
Kushoto mwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru ni makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru wakati wa baraza la Halmashauri hiyo.
Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Ndg. Maarufu Mkwaya akiwasilisha mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Katika siku ya kwanza ya Mkutano ,baraza la Halmashauri ya Meru lilikabidhi cheti cha kutambua mchango wa Shirika la See way Tanzania ambalo makao yake makuu yapo Kata ya Imbaseni kwa kutekeleza miradi ya zaidi ya milioni 90 katika Shule ya Msingi ya Imbaseni ikiwa ni ujenzi wa Vyumba 6 vya madarasa, Vyoo vya walimu matundu 4, Kufanya ukarabati mkubwa wa vyoo vya wanafunzi matundu 17 , Kutengeneza madawati 100 na kuwezesha watoto toka mazingira magumu kwa kuwanunulia sare na vifaa vya Shule.
Pia shirika hilo linaendelea na Ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Kiwawa kwa awamu ambao mpaka sasa ujenzi ulio fanyika ni wa Jengo la Utawala lenye ofisi zote stahiki, ujenzi wa Vyumba 4 vya madarasa umefikia hatua ya upauaji na vyumba vingine 4 vya madarasa vipo hatua ya msingi, ujenzi wa Vyoo vya wanafunzi matundu 18 umefikia hatua ya lenta na ujenzi wa Maabara 2 za sayansi upo hatua ya msingi.
Waheshimiwa Madiwani wakati wa Mkutano wa baraza.
Kushoto ni Afisa Tarafa,Tarafa ya Poli Ndg. Dominick Rweyemamu na kulia ni Afisa Tarafa ,Tarafa ya Mbuguni Ndg. Abdallah Ten .
Diwani viti maalum Kata ya Nkoanrua Eveline Kaaya akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza.
Mheshimiwa Diwani kata ya Akheri Romani Kibanda wakati wa Mkutano wa baraza.
Mhe.Diwani Kata ya Nkoandua Isack Kanuya akizungunza wakati wa Mkutano wa Baraza.
Diwani Kata ya Maji ya chai Anderson Pallangyo akizungumza wakati wa baraza la Halmashauri.
Baadhi ya wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na wawakilishi wa wakuu wa Idara wakati wa mkutano wa baraza.
Diwani kata ya Kikwe Paul Shango akizungu mza wakati wa Mkutano wa Baraza.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa