Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Meru, lapitisha rasimu ya Mpango wa Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha ujao 2022/2023, kiasi Cha Shilingi bilioni 55.5 ikiwa ni ongezeko la asilimia 8% ikilinganishwa na bajeti ya Mwaka wa fedha unaoendelea.
Akizungumza wakati wa mkutano huo,Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Meru Mhe.Jeremia Kishili, amethibitisha baraza hilo kupitisha Mpango wa bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka ujao wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 55.5 kwa mchanganuo wa ,mapato ya ndani Shilingi Bilioni 6.7, Ruzuku ya Mishaara ya Watumishi Shilingi Bilioni 36.18, Ruzuku ya kawaida Shilingi Bilioni 1.18 na miradi ya maendeleo Shilingi Bilioni 11.45.
Aidha Mhe.Kishili amemshukuru Rais.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za maendeleo katika sekta ya Elimu, afya, Maji na barabara katika Halmashauri ya Meru. Pia amewapongeza wataalam wa Halmashauri hiyo wakiongozwa na Mkurugenzi Zainabu kwa Kushirikiana vyema kuleta maendeleo katika Halmashauri hiyo sambamba na wadau mbalimbali wa maendeleo na kutoa wito ushirikiano huo kuwa endelevu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwl.Zainabu Makwinya amesema ongezeko Hilo la asilimia 8% ya bajeti ya Mwaka 2022/2023 inatokana na uibuaji wa vyanzo vipya vya mapato na hali halosi ya makusanyo hadi Disemba 2021, ambapo ametoa mfano bajeti ya mapato ya ndani yasiyofungiwa yameongezeka kwa asilimia 44% kutoka Shilingi Bilioni 2.18 2021/2022 hadi Bilioni 3.1 Mwaka wa fedha ujao 2022/2023
Mwl.Makwinya amesema, kipaumbele chake ni ukusanyaji wa mapato yatakayotumika kuwaletea Wananchi maendeleo ambapo katika mikakati ya kufanikisha hilo wameshakutana na wenyeviti wa Vijiji na watendaji wa Kata na wanataraji kukutana nao tena na Watendaji hao kwa pamoja na wenyeviti wa vijini na watendaji wa vijiji Ili kuhakikisha mapato yanakusanywa.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango ameipongeza Rasimu ya bajeti ya Halmashauri ya Meru kwa Mwaka 2022/2023 kwa kiasi kikubwa inakidhi hali halisi ya Halmashauri hiyo. Pia amewakumbusha Waheshimiwa Madiwani kujiandaa na Swala la Sensa ya watu na Makazi linalotarajiwa kuanza mwezi Agasti 2022.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Waheshimiwa Madiwani mbali na kuipongeza rasimu hiyo kuwa na tija kwa wanameru wameonesha kuendelea kushirikiana kuwaletea Wananchi wa Meru maendeleo ambapo wameamua Shilingi Milioni 26 katika bajeti inayoendelea , zilizokuwa zimetengwa kama fedha za Utengenezaji wa miundombinu ya barabara kila Kata kwa mgao wa Shilingi Milioni Moja kupeleka kuchimbua korongo la Mto nduruma ambalo ni changamoto kubwa kwa Wananchi wa Kata ya Shambarai Burka , Maroroni na Mbuguni.
"Tunashukuru sana Baraza la Madiwani kuafiki fedha Milioni 26 kutatua changamoto hii ya korongo la mto Nduruma kwani wakati wa Mvua barabara zinajaa Maji Kinamama wanapata sana tabu na wanafunzi pia" Mollel Diwani wa Kata ya Shambarai Burka .
Ikumbukwe
Mpango huo wa bajeti umeandaliwa kwa mujibu wa kifungu Na. 11 cha sheria ya Sheria ya Bajeti Na. 21 ya mwaka 2015 pamoja na Kanuni zake, maelekezo na mwongozo wa kitaifa maandalizi ya Bajeti, unaoelekeza kupokea mapendekezo na vipaumbele kisekta kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata, Idara na Vitengo vya halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa