Shirika lisilo la kiserikali la "Cross Talent Share International"(CTSI) limetoa msaada wa vitu vyenye thamani ya sh.Mil 5.5 katika shule ya Sekondari King'ori baada ya kupata majanga ya kuunguliwa na Bweni la wasichana.
Mwakilishi wa shirika la CTSI Bw. Justin Mwaisemba amekabidhi msaada huo shuleni hapo leo ikiwa ni pamoja na Magodoro 66, Mashuka 150 pamoja na vyandarua 66 kama sehemu ya kuwaandalia mazingira mazuri ya kusoma kwa kipindi ambacho shule zimefunguliwa.
"Mkurugenzi wa CTSI Bw. Hyeonseok Kim amewapa pole sana na ametamani sana angeshiriki katika zoezi hili lakini amepata dharura na majukumu nchini Korea na kunituma nimwakilishe ili kukabidhi msaada huu. Amesema Mwaisemba .
Aidha, ameeleza kuwa wao kama shirika wanaendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Meru na kwa sasa wanajiandaa kwa ajili ya kusaidia kukarabati bweni lililoungua.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Meru Mwl. Zainabu J. Makwinya ametoa shukrani kwa shirika hilo ambalo limekuwa likitoa ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Meru.
" Natoa shukrani kwa Shirika la CTSI kwa kutusaidia kurudisha furaha kwa wanafunzi hawa kwani mara tulipopata tatizo walikuwa tayari na waliahidi kutoa msaada huo shule itakapofunguliwa.
Ameeleza kuwa CTSI wamekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani wamechangia miradi ya maendeleo mingi katika Halmashauri ya Meru kama vile Ujenzi wa Madarasa, Vituo vya Afya na Zahanati.
Diwani Kata ya Malula Mhe. Lukumbwe Ndossi ameeleza kuwa chanzo cha Moto bado hakijafahamika lakini wameanza kuchukua tahadhali ya majanga ili yasitokee tena. Pia, ametoa shukrani kwa Mfadhili huyo kwani kitendo hicho kitawasaidia wanafunzi kupata utulivu katika masomo.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa