Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Kaganda ametoa wito kwa wananchi kutunza vyanzo vya maji na mazingira ambapo pia amewataka wanaofanya shughuli za kibinadamu katika milima kuacha mara moja kwani Serikali wilayani humo haitowafumbia macho.
Mhe.Kaganda amesema hayo wakati akiwaongoza wananchi wa Kata ya Mbuguni Halmashauri ya Meru, kupanda miti kwenye kingo za korongo la mto Nduruma ambalo Serikali ya awamu ya Sita ikiongozwa na Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan ilitoa zaidi ya Milioni 200 za kufukua korongo hilo na kutatua changamoto ya mafuriko iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa Kata hiyo ya Mbuguni na Shambarai Burka.
Mhe.Kaganda amesema Wilaya ya Arumeru imebarikiwa kuwa na vyanzo Vingi vya maji vinavyoanzia milimani, hivyo wananchi hawana budi kuvitunza kwa manufaa yao na manufaa ya wengine " Wazee wetu walitunza vyanzo hivi nasi tunapaswa kuvitunza kwa ajili ya kizazi kijacho"amehimiza Mhe Kaganda
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwl Zainabu Makwinya amesema Halmashauri hiyo inahakikisha inaunga mkono juhudi za Serikali katika agenda ya utunzaji mazingira na vyanzo vya maji, ambapo awali kupitia mapato yake ya ndani Waheshimiwa madiwani waliridhia kutoa Milioni 26 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwenda kuchimbua Korongo hilo la mto Nduruma.
Nao Waheshimiwa Madiwani wa Kata za Shambarai na Mbuguni ambazo awali zilikuwa zikisumbuliwa na mafuriko wameishukuru Serikali kufukua Korongo hilo na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji.
Tito Kitomari kutoka Bonde la Pangani ametoa Wito kwa jamii kutunza vyanzo vya maji vilivyopo kwani hakuna mbadala wake ambapo amebainisha Bonde la Pangani kuendelea kushirikiana na Jamii na Serikali katika utunzaji wa vyanzo vya maji.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa