Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Kaganda ametoa maagizo kwa wasimamizi wa Vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya Jamii kuhakikisha wanakuwa waaminifu katika ukusanyaji wa Fedha za miradi ya maji na kufanya kazi kwa bidii.
Mkuu wa Wilaya hiyo ametoa maelekezo katika Mkutano Mkuu wa nusu mwaka kwa Vyombo vya watoa huduma ya Maji ngazi ya Jamii (CBWSOs) ( BI - ANNUAL COMMUNITY OF PRACTICE MEETING) RUWASA Wilaya ya Arumeru uliofanyika katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii kilichopo Tengeru.
"Ninawaagiza kufanya kazi kwa bidii na kuwa waaminifu katika ukusanyaji wa fedha za miradi ya maji pamoja na usimamizi wa ukarabati mkubwa na mdogo katika miradi hiyo. Aidha, hatua zitachukuliwa kwa wale wote watakaokiuka na kuvunja taratibu. Hili ni pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa wananchi wanaoharibu vyanzo vya maji" Alisema Kaganda.
Vilevile Mhe. Kaganda ameeleza kuwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 imezingatia na imeelezea umuhimu wa maji ambapo Sura ya 3 Ibara ya 97 ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi imeeleza kuwa maji ni msingi wa uhai wa binadamu na injini ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii hivyo upatikanaji wa uhakika wa huduma ya maji safi na salama na usafi wa mazingira huchangia sana katika kuzuia magonjwa na hivyo kuimarisha afya na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.
Meneja RUWASA Mkoa Wa Arusha Eng. Joseph Makaidi ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maji kwa Wilaya ya Arumeru. Pia amemshukuru Mhe. Kaganda kwa ufuatiliaji na utatuzi wa changamoto za miradi ya maji.
Hata hivyo Meneja Wa RUWASA Arumeru Eng. Shabib Wazir amewasilisha changamoto wanazokutana nazo ikiwa ni pamoja na baadhi ya Taasisi kutolipa bili za maji, wananchi kukataa kufungiwa mita za maji na Serikali kutoshirikishwa katika miradi ya ufadhili ili iweze kusimamiwa na Serikali.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa