Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari leo tarehe 7 Januari, 2025 wametoa mafunzo ya uhakiki wa taarifa za Anwani za Makazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Elimu Maalum Patandi - Tengeru.
Katika Ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Amir Mkalipa ambaye pia ni mgeni rasmi katika Ufunguzi wa mafunzo hayo, amewataka Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji kuhakikisha baada ya mafunzo hayo waende kuhamasisha wananchi katika maeneo yao kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuhakiki anwani za makazi.
"Niwaombe Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji kutoa ushirikiano mkubwa katika zoezi hili kwa kushirikiana na Watendaji wa Kata na Vijiji ili Wananchi wetu wafahamu kuwa hii ni fursa kwao kuhakiki taarifa zao lakini pia itarahisisha kuyatambua maeneo yetu kirahisi tofauti na njia zilizotumika awali." Amesema Mkalipa.
Aidha, Mhe. Mkalipa amewataka Wenyeviti hao kutoa taarifa kwa kamati ya Usalama ya Wilaya endapo kama watatokea watu watakaotaka kukwamisha zoezi hilo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Vilevile, Mkuu huyo amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Meru kusimamia zoezi hilo kikamilifu kwa kushirikiana na TARURA na TANROADS kuhakikisha Barabara zote zinakuwa na nguzo za majina ya Barabara.
Washiriki katika Mafunzo hayo ni Wakuu wa Taasisi wakiwemo TANROADS na TARURA, Wakuu wa Idara na Vitengo Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji pamoja na Watendaji wa Kata na Vijiji pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambao ndio walioendesha mafunzo hayo.Fungua Hapa Kutazama Video
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa