Na ARUSHA MEDICAL BLOG.
Mada hii inaelenga kutoa elimu juu ya maradhi ya ini ambayo kwa kitaalamu huitwa mwako wa Ini yaani Hepatitis.
Ini ni ogani muhimu katika mwili wa binadamu inayofanya kazi kadhaa ikiwemo kuandaa virutubisho/dawa mbalimbali vitokanavyo kwenye chakula pindi kiingiapo mwilini,kuchuja damu na kupambana na magonjwa.
Mwako wa Ini ni mabadiliko yanayotokea kwenye ini katika hali ya kupambana na athari za ugonjwa zinazoletwa na virusi,sumusumu au kemikali mbalimbali ziingiazo mwilini.
Hali hii huweza kuisha au kuendelea na kusababisha makovu ya kudumu katika ini na hata kupelekea kupata kansa ya ini.
Mada hii itaangazia kuhusu ugonjwa wa ini utokanao na virusi(viral hepatitis) kwani kwa mtazamo wangu bado elimu hii kwa jamii ipo chini kiasi cha kushuhudia wagonjwa wa ini wakifika hospitali katika hatua za mwisho.
Kulingana na uwezo wa hospitali zetu na pia kwa uwezo wa kiuchumi wa jamii yetu tunashindwa kutibu au kuboresha maisha ya wagonjwa hawa.
Aina za Virusi vya ugonjwa wa ini
Kwa umuhimu wa afya ya jamii zipo aina kuu tano za virusi vya ugonjwa wa ini(hepatitis Virus),Ambazo ni pamoja na aina A,B,C,D na E.
Virusi aina ya A,B na C ndivyo huonekana mara nyingi kwa waathirika wa ugonjwa huu wa ini.Virusi aina ya B na C husababisha ugonjwa wa ini wa kudumu na hivyo kupelekea makovu makubwa kwenye ini au kansa ya ini.
Virusi aina ya B,C na D huambukizwa kupitia njia ya damu huku vile vya A na E huambukizwa kwa njia ya kumeza au kunywa vyakula vyenye virusi hao.
Virusi aina A(HAV)
Virusi vya aina A husambazwa kwa njia ya kula au kunywa vyakula vyenye kinyesi cha muathirika wa virusi hivi.
Inakadiriwa kuwa kiwango cha vifo vitokanavyo na virusi hivi ni chini ya asilimia 0.1% kwa mwaka nchini Tanzania na huathiri zaidi watoto wa umri wa miaka 1 hadi 4(Global disease burden).
Mara nyingi maambukizi yake huendana na maambukizi ya magonjwa mengineyo ya kuhara,pia virusi hivi huweza kuenezwa na wahudumu wa kwenye hoteli na mighawa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mama ntilie ,Bado hakuna ufuatiliaji wa kina hasa katika kuhakikisha watoa huduma za vyakula wanapimwa mara kwa mara kabla ya kupewa leseni za kufanya kazi za kuuza au kuhudumia kwenye mighawa.
Virusi hivi hupelekea ugonjwa wa muda mfupi (ingawa unaweza kuhatarisha maisha) na baadae kuisha na kumuacha mgonjwa akiwa na kinga.
Kinga dhidi ya HAV inaweza kutolewa ili kupunguza makali au athari za ugonjwa.
Virusi aina ya B(HBV)
Virusi hivi huambukizwa kwa njia ya muingiliano wa damu au majimaji mengine ya mwili mfano kwa kujamiiana,kuwekewa damu yenye virusi,kujichoma sindano zenye kubeba virusi,kujidunga kwa wale wanaotumia madawa ya kulevya n.k.
Pia huweza kuambukizwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua.
Inakadiriwa kuwa virusi hivi husababisha vifo kiasi cha asilimia 0.6 kwa mwaka (Global disease burden) ingawa kiwango hiki kinaweza kuwa ni kidogo kulinganisha na uhalisia.Hii inatokana na uelewa mdogo wa jamii kuhusu ugonjwa na upimaji pamoja na ufuatiliaji wa ugonjwa huu unaofanywa na watumishi wa afya.
Maambukizi ya virusi vya HBV huendana na maambukizi ya virusi vya ukimwi hivyo kuna uhitaji wa kufuatilia na kuweka mbinu zinazoshabihiana katika kukabili magonjwa haya.
Chanjo dhidi ya virusi vya HBV hupatikana kwa urahisi.
Virusi vya aina C(HCV)
Huweza kuambukizwa kupitia njia ya damu na mara chache kwa njia ya kujamiiana.
Virusi hivi havina Chanjo.
Virusi vya aina D(HDV)
Virusi hivi huathiri wale ambao wameathiriwa na virusi aina ya B.
Maambukizi ya virusi B na D huweza kupelekea athari kali zaidi kulinganisha na B pekee.
Chanjo dhidi ya virusi B husaidia kujikinga dhidi ya athari za maambukizi ya virusi D.
Virusi vya E(HEV)
huambukizwa kwa njia ya kula au kunywa vyakula vilivyoathiriwa.Aina hii hugundulika katika ufuatiliaji wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa ini.
Dalili za Ugonjwa
Dalili za ugonjwa wa ini kutokana na virusi zaweza kufanana na dalili za magonjwa mbalimbali.Mara nyingi dalili za ugonjwa wa ini huweza kutokea ghafla,dalili hizo hujumuisha :
Kinga
Chanjo ya Virusi aina A,B na E huweza kuchomwa ili kukinga dhidi ya maradhi ya ini.
Chanjo ya virusi A hutolewa kwa watoto chini ya mwaka mmoja na ile ya Virusi B hutolewa kwa watoto chini ya miaka 18.
Pia chanjo hizo huweza kutolewa kwa wasafiri wanaoenda kwenye maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi.
Njia muhimu za kujikinga na maambukizi ni pamoja na kunawa mikono kabla ya kuhudumia chakula,kutochangia sindano,viwembe au miswaki,kutumia kinga wakati wa kujamiiana.
Uchunguzi
Kwa ufupi uchunguzi wa virusi vya hepatitis hufanyika kwa njia za maabara ambapo damu hufanyiwa uchunguzi kama ina vimeleakinga vya virusi (antigens) au vimeleakinga(antibodies) vya mwili.
kupitia uchinguzi huu wataalamu wa afya hufanikiwa kugundua uwepo wa ugonjwa kwa wakati wa kipimo au kama mtu aliwahi kuathirika hapo awali.
Pia vipimo vya uwezo wa ini kufanya kazi vinaweza kusaidia katika matibabu ya mgonjwa.
Matibabu
Ugonjwa huu huweza kuisha bila matibabu yoyote katka kipindi cha majuma manne hadi sita,lakina pia huweza kuwa ni wa kudumu(kirusi B).
Matibabu yake huweza kujikita katika kukabili dalili.
Dawa za kufubaza virusi huweza kutumika mfano Tenofovir au lamivudine.
Katika hatua za mwisho za ugonjwa yaani ini kushindwa kufanya kazi ,kubadilishwa kwa ini inaweza kuwa ni njia pekee ya matibabu.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa