HAKIKISHENI SHULE ZOTE ZINAKUWA NA BUSTANI ZA MBOGA MBOGA - KAGANDA
Imewekwa: February 9th, 2024
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda ametoa maelekezo kwa Wakuu Wa Divisheni ya Elimu ya awali Msingi na Elimu Sekondari Halmashauri ya Meru, kuhakikisha shule zote zinakuwa na Bustani za mbogamboga.
Mhe. Kaganda ametoa maelekezo hayo katika kikao cha Tathmini ya Lishe Wilaya cha kujadili taarifa ya Lishe kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2023.
" Afisa Elimu Msingi na Sekondari hakikisheni shule zote wanatengeneza bustani za mbogamboga na shule zenye maeneo makubwa wahamasishwe kufanya kilimo cha mazao kama Mahindi na Maharage". Alisema Kaganda.
Aidha, Afisa Lishe Wilaya Bi. Rehema Lema alieleza kuwa, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri katika bajeti yake iliidhinisha kiasi cha shilingi 57,459,500.00 kutoka Mapato ya Ndani na Fedha hizo zilitengwa kwa ajili ya kutekeleza shughuli za Lishe ikiwa ni utekelezaji wa kutenga shilingi 1000 kwa kila mtoto aliye na umri wa chini ya miaka mitano.
Hata Hivyo, Mhe. Kaganda ametoa Maelekezo kwa Mratibu wa Lishe Wilaya kuhakikisha Mafunzo ya Afua za lishe yanatolewa kwa Watendaji wa Kata wote ili waweze kusimamia utekelezaji wa Mkataba wa Afua za Lishe.
Vilevile, Kamanda wa Polisi Wilaya SSP. Joseph Mtenga alishauri kuwa Shule ambazo Wazazi hawachangii chakula wapewe Elimu na tujifunze kutoka kwenye Shule zinazotoa chakula ili nao wachangie chakula.