Halmashauri ya Meru wilaya ya Arumeru imeshika nafasi ya Tano kitaifa na ya kwanza kimkoa na kuzibwaga halmashauri zote sita za mkoa wa Arusha katika matokeo ya kidato cha pili yaliyotoka mapema wiki hii.
Akizungumza na mwandishi wetu Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Meru mwalimu Damari Mchome amesema kuwa Halmashauri ya Meru imeshika nafasi ya Tano kati ya halmashauri 175 za Tanzania bara na kuifanya halmashauri hiyo kushika nafasi ya kwanza kimkoa.
Afisa Elimu Mchome ameongeza kuwa kati ya wanafunzi 5,096 waliofanya mtihani wa kidato cha pili mwa 2017 wanafunzi 1,278 wamepata daraja la kwanza, 760 daraja la pili, 874 daraja la tatu na 1,902 daraja la nne kuifanya alama ya ufaulu ya GPA ya 3.185
Akielezea siri ya ufaulu huo Mchome amesema kuwa halmashauri ina walimu wa kutosha kwenye masom ya sanaa pamoja na sera ya elimu bila malipo inayosababisha wanafunzi kuhudhuria masomo bila usumbufu wa kudaiwa "Baada ya serikali kutoa elimu bila malipo wanafunzi wamekuwa wakihudhuria darasani bila kukosa tofauti na hapo awali walipokuwa wanakosa masomo kwa kushindwa kulipa ada na michango mingine jambo lililochangia ufaulu kwa wanafunzi hao" amefafanua Afisa Elimu
Hata hivyo Halmashauri imepokea jumla ya wanafunzi 5,404 wa kidato cha kwanza mwaka 2018 wavulana 2,540 na wasichana 2,862 kwenye shule 29 za serikali.
Afisa Elimu taaluma Abernego Mlokozi amesema kuwa wanafunzi hao 5,404 wamegawanywa kwenye mikondo 92 na tayari wanafunzi hao wameanza mafunzo ya awali ikiwemo matumizi ya lugha ya Kiingereza yatakayofanyika kwa wiki nane kwa lengo la kuwajengea msingi wa lugha hiyo itakayotumika kufundishia masomo yote kasoro somo la Kiswahili.
Mulokozi ameongeza kuwa halmashauri imepokea vitabu vya kufundishia mafunzo hayo ya awali kwa uwino wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa