Halmashauri ya Wilaya ya Meru imefanya kongamano la wadau wa mazingira ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya siku ya mazingira duniani ambapo kitaifa imefanyika jijini Dodoma na mgeni rasmi ni Mhe.Kassim Majaliwa, waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungana wa Tanzania.
Mgeni Rasmi wa kongamano hilo Mhe.Lucas Kaaya diwani wa Kata ya King'ori na Mwenyekiti wa kamati ya uchumi ,ujenzi na mazingira ametoa wito kwa jamii, kila mmoja kutambua ni mdau wa mazingira na anawajibu wa kuhakikisha mazingira yanakuwa salama muda wote kwani hakuna maisha bila mazingira salama "mazingira yaliyohifadhiwa ndio uchumi wa taifa, nitoe wito kwa watendaji wa serikali na wananchi kutimiza wajibu wao kutunza mazingira kwa kutii sheria za mazingira na kutoharibu ikolojia" amehimiza Mhe.kaaya
Nao wadau wa mazingira wametoa elimu juu ya umuhimu wa kutunza mazingira sambamba na madhara ya plastiki ambapo Mtafiti Erick Kato kutoka Taasisi ya Nelson Mandela amesema mbali na jitihada za serikali kudhibiti madhara ya matumizi ya plastiki kwa kupiga marufuku matumizi ya mifuko, bado nguvu zaidi inahitajika katika kudhibiti matumizi ya plastiki inayoleta madhara ardhini, kwa wanyama ,binadamu na hewa kwa ujumla.
Aidha. Mtafiti Kato amesema madhara ya plastiki ndogondogo (microplastics) kwa Binadamu ni pamoja na kuathiri mfumo wa uzazi na hewa ambapo amebainisha plastiki huingia kwa binadamu kupitia mbogamboga , viazi ,karoti pamoja na kutumia vyombo vya plastiki kuweka vyakula vya moto nk. Aliongeza kwamba bado elimu ya uelewa juu ya microplastics inahitajika sana kwa jamii na kuwaomba wadau kubuni njia mbadala ya matumizi ya plastiki na kusambaza elimu zaidi juu ya madhara ya plastiki hasa zile ndogo microplastics.
Lewis Nzali ambaye ni
Meneja wa Baraza la mazingira (NEMC ) kanda ya kaskazini, ametoa wito kwa jamii kutumia fursa ya taka ni pesa kuchakata taka kuzaliza bidhaa rafiki kwa mazingira " nitoe wito kwa jamii kutenganisha taka ili kurahisisha matumizi yake kwani taka za mabaki ya chakula hutumika kutengeneza mboji pia taka za plastiki huchakata kutengeneza bidhaa kama viti/ benchi za kupumzika hivyo kupunguza uharibifu wa mazingira"ameeleza Nzali
Mhandisi Arafa Magidi ambae ni mkuu wa kitengo cha mazingira Bonde la Pangani ametoa wito kwa jamii kuishi kwenye Kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya Mazingira duniani "Tanzania ni moja tu,tunza Mazingira " ambapo amebainisha watanzania wanapaswa kutunza vyanzo vya maji vilivyopo tanzania kwani hakuna namna ya kuchukua vyanzo kwenye sayari nyingine.
Enock Chengula kutoka Kijani Pamoja ametoa wito kwa jamii kushiriki kutunza mazingira kwa kupanda miti ambapo wao Kijani Pamoja katika kufanikisha hilo wameanzisha programu ya kuhamasisha jamii kupanda miti , ambapo hulipa Shilingi mia nne kwa kila mti mtu atakaoupanda na kuutunza ndani ya miezi mitatu "tunakupa Mche unautunza ndani ya miezi mitatu tunakulipa shilingi mia nne, kigezo kikubwa ni mti ukue "amefafanua Chengula.
Mkuu wa Idara ya Usafi na mazinga halmashauri ya Wilaya ya Meru Ndg.Charles Makama ametoa wito kwa wadau kutoa elimu kwa jamii ili kuwa na ushiriki wa pamoja katika kutunza mazingira.
Naye Afisa Maliasi na utalii halmashauri ya Meru Ndg. Charles Mungure amesema Halmashauri hiyo imeweka mikakati ya kutunza mazingira kwa kudhibiti ukataji miti hovyo ambapo uongozi wa Kijiji unakuwa mstari wa mbele kudhibiti hilo kwani ili mwananchi apate kibali cha kukata mti kutoka Halmashauri anakuwa na mhutasari wa kikao cha kijiji kilichoridhia.
Mhamasishaji na mdau wa mazingira Ndg.Vicent Uhenga toka VOYOTA amesema wao huhamasisha jamii wakati wa kusherekea siku za kuzaliwa kupanda idadi ya miti inayolingana na umri wanaotimiza. Pia ametoa rai miti ya asili kizingatiwa katika mazoezi ya kupanda miti .
Dkt. Aman Sanga ambaye amemwakilisha Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo amewashukuru wadau wote walioshiriki maadhimisho hayo ya wiki ya mazingira ikiwa ni pamoja na Baraza la Taifa la uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kaskazini ,Bodi ya Maji Bonde la Pangani, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, ANAPA,TICD, Jobopportunity Change for future, Dunia Salama Foundation, Twice Foundation, Awe College, Twice Foundation na Ngarasero Mountain lodge.Change for future,Hakiki ndoto zako Organizaton,Kisali na Seu Tv,Usa -River Malihai club,Kijani Pamoja,Dunia Salama Foundation,Duluti Green foundation,Trial Tabzanis,ECH East Africa,Zumbi Family,Kilimanjaro Expert,Mojifa (ECA) na Kwalenawe Cultural
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa