Na. Annamaria Makweba.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Nurdin Babu amewataka wananchi wote kuchagua viongozi bora katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Oktoba, 2024.
Mhe. Babu ambaye ni Mgeni Rasmi katika ufungunzi wa Maonyesho ya Nanenane ya Kanda ya Kaskazini inayounda Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara amewataka wananchi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uchaguzi na kuchagua viongozi bora ili waweze kuwaongoza vyema.
Aidha, Mhe. Babu ameeleza kuwa Uchaguzi utakuwa huru na haki na kuzingatia taratibu za kiusalama katika maeneo yote yatakayofanyika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Hata hivyo, Mhe. Mgeni rasmi katika hotuba yake ameeleza kuwa, kwa kipindi cha mwaka wa Fedha 2023/2024 Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka nguvu kubwa katika kuboresha Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kwa Kanda ya Kaskazini imenufaika katika utoaji wa mbolea ya Ruzuku kwa ajili ya kuongeza tija kwenye kilimo ambapo jumla ya Tani 61,400 zimetolewa kwa wakulima wa mikoa 3 ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara yenye thamani ya sh. Bilioni 85.96.
Pia, kwa upande wa uboreshaji wa Miundombinu ya Umwagiliaji Mhe. Babu ameeleza kuwa Serikali imeweza kujenga na kukarabati mifereji na mabwawa yenye thamani ya shilingi Bilioni 62.4 . Ambapo kwa Mkoa wa Manyara Bilioni 15.6, Arusha Bilioni 38.4 na Kilimanjaro Bilioni 8.4.
Vilevile, kwa upande wa Mifugo ameeleza kuwa jumla ya Ng'ombe 44,970 wamehimilishwa kwa mbegu bora za kisasa.
Ameeleza kuwa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya yote haya ili kila Mtanzania anayeweza kufanya kazi afanye katika maeneo hayo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mhe. Babu amewataka wananchi wote kutembelea mabanda na kupata elimu itakayowasaidia kufanya shughuli zao za kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kuongeza uzalishaji.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa