Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango wamefanya ziara ya Ukaguzi wa Mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Ufundi stadi (Veta) kinachojengwa Kata ya Uwiro Katika Halmashauri ya Meru.
Ziara hiyo ni utaratibu wa Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango kukagua Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri kwa kila robo Mwaka, ambapo ukaguzi huu ni wa robo ya kwanza Kipindi cha Mwezi Julai- Septemba 2023 kwa mwaka wa Fedha 2023/2024.
Ukaguzi huo umehusisha Wataalam mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Meru ambapo kwa pamoja wamekagua Mradi huo unaojengwa kwa mfumo wa "Force Account" kupitia Kamati tatu za Chuo Cha Ualimu Patandi chini ya Usimamizi wa Mhandisi Mshauri Mponjoli Zakaria kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi Dar- es- Salaam (ARU).
Mradi wa Ujenzi wa chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Katika Kata Uwiro ni moja kati ya utekelezaji miradi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ambapo Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan imekusudia kujenga Vyuo vya Ufundi stadi 63 vya Wilaya na Kimoja cha Mkoa.
Mkuu Wa Chuo cha Ualimu Elimu Maalum Patandi Lucian E. Segesela Katika taarifa yake ameeleza kuwa Serikali imepanga kutekeleza Mradi huo kwa awamu mbili kwa kujenga majengo kumi na nane ambapo tisa yatajengwa sasa na mengine yatajengwa awamu ya pili.
" Kwa sasa majengo yanayojengwa ni Jengo la Utawala, Majengo 3 ya Karakana, jengo la nyumba ya Mkuu wa Chuo, Jengo la madarasa, jengo la choo, jengo la kibanda cha Mlinzi na Jengo la kupokelea umeme.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mhe. Jeremia Kishili na Wajumbe wa Kamati ya Fedha kwa niaba ya Baraza la Halmashauri wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa ya ujenzi wa chuo cha ufundi stadi (VETA) katika Halmashauri ya Meru.
Hata hivyo, Mhe. Godson Majola Mjumbe wa Kamati hiyo ametoa angalizo kuwa, Kamati za ujenzi ziongeze umakini katika kusimamia ujenzi wa Chuo hicho ikiwa ni pamoja na kuweka nyaraka zote za mradi.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa