Kamati ya Siasa Wilaya ya Kichama ya Meru imewataka Wahandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru kuwatumia mafundi wenye ujuzi na wazalendo katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya Serikali sambamba na kufuatilia kwa karibu ujenzi na kuhakikisha mafundi wamefanya kazi kwa mujibu wa BOQ na maelekezo ya kitaalam kabla ya kulipa fedha kwa kila awamu na fedha za zuio.
Kamati ya Siasa imeelekeza Wahandisi kufuatilia na kuwasimamia mafundi kwa ukaribu ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vilivyowekwa. Maelekezo hayo yametolewa kutokana na changamoto ndogo ndogo zilizobainika katika ukaguzi wa baadhi ya Miradi .
Hayo yamejiri wakati Kamati ya Siasa ilipotembelea na kukagua ujenzi wa vyumba vya Madarasa matatu(3) katika Shule ya Msingi Kerikenyi ambao umefadhiliwa na Serikali Kuu kupitia Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R).
Aidha, Kamati imewashukuru wafadhili wa miradi mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru na kutoa Wito kwa wafadhili hao kuwatumia Wananchi katika utekelezaji wa miradi ili miradi hiyo kuwa na tija zaidi kwa kutekelezwa kwa gharama nafuu na kuongeza wigo wa kutekeleza miradi mingi zaidi.
Kamati imepongeza ujenzi wa Vyumba manne (4) vya Madarasa katika Shule za Sekondari Mbuguni na Majengo na ambayo yameonekana kusimamia vyema na wahandisi wa ujenzi ambapo Kamati imepongeza uongozi wa Vijiji, Kata na Halmashauri kwa ushirikiano na usimamizi mzuri wa miradi.
Pia. Kamati ya Siasa imempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Meru Ndg.Emmanuel Mkongo kwa msimamo imara wa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Serikali katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya katika Halmashauri hiyo .
Ikiwa ni siku ya 3 na ya Mwisho ya ziara ya Kamati ya siasa baada ya kutembelea na kukagua miradi 18 katika sekta za Afya, Elimu, Kilimo, Ufugaji, Uchumi na Uzalishaji mali, Kamati imeelekeza Halmashauri kuhakikisha inaendelea kuunga Mkono juhudi za Wananchi kwa kuchangia ujenzi wa miradi iliyoanzishwa na Wananchi sambamba na kuongeza mikopo kwa Vikundi vya Wanawake Vijana na Watu wenye ulemavu vinavyotumia mikopo kwa tija na kurejesha kwa wakati. Aidha, Kamati imetoa rai kwa Viongozi wa Vitongoji, Vijiji, Kata na Chama katika ngazi ya Matawi na Kata kuwahamasisha Wananchi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususani ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya katika Zahanati ambazo hazina nyumba hali inayokwamisha utoaji wa huduma ya afya.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa