Wananchi wa Kata ya Maroroni ,Halmashauri ya Wilaya ya Meru waendelea kuonyesha jitihada za kizalendo kushiriki kikamilifu katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha huduma za afya sambamba na utoaji elimu bila malipo.
Hayo yamedhihirika katika hafla ya Serikali ya kijiji cha Migandini kilichopo Kata ya Maroronii, kukabidhi Madawati 27 mapya kwaajili ya wanafunzi wa shule ya Msingi Migandini.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho Mhe. Christopher Pallangyo amesema wananchi wamehamasika kushiriki shughuli za maendeleo haswa kwenye sekta ya elimu baada ya Serikali kutoa elimu bila malipo.
Pallangyo amesema Serikali ya kijiji hicho katika kuunga mkono utoaji wa elimu bila malipo imechangia zaidi ya milioni 2 kwa kutumia rasilimali miti na rasilimali watu kutengeneza madawati mapya 27 pamoja na kukarabati madawati 16.
Pallangyo, amesema baada ya kupata taarifa ya uhaba wa madawati katika shule hiyo waliamua kutumia miti ya kijiji kutengeneza mbao na kuwashirikisha wananchi wenye ujuzi wa ufundi kujitolea kutengeneza madawati hayo bila malipo.
Pallangyo ameongeza kuwa, Wananchi wa kijiji hicho wamekua mstari wa mbele kushiriki kujiletea maendeleo ambapo kwa kushirikiana na wadau wamefanya ujenzi wa zahanati ya kijiji ambayo imefikia hatua ya lenta, Pia wamekubaliana kushiriki katika ujenzi wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu .
Mwl.David Kyara ambaye ni mwalimu mkuu shule ya Msingi Migandini amesema shule hiyo yenye wanafunzi 400 ilikuwa na uhaba wa madawati 33, hivyo madawati yaliyokarabati yatapunguza uhaba na kubakiwa madawati 6 ambapo uongozi wa kijiji umeahidi kutengeneza.
Diwani wa Kata ya Maroroni Mhe.Yona Nnko amepongeza utendaji wa mwenyekiti wa kijiji cha Migandini katika gurudumu la kuharakisha maendeleo sambamba na ushirikiano katika ngazi ya Kata.
Mhe. Yona amesema anajivuni wananchi wa Kata hiyo kwani wamekuwa mstari wa mbele katika kujiletea maendeleo, ambapo jitihada zao ziliungwa mkono na Baraza la Halmashauri hiyo, lililopitisha ujenzi wa kituo cha afya kitakacho gharimu kiasi cha Sh.Milioni 400 kupitia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo kutekelezwa katika kata hiyo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,Ndg.Exaud Kimaro ambaye pia ni Afisa elimu maalum, amepongeza juhudi za wananchi na uongozi wa kijiji hicho na kuahidi kuwasilisha changamoto za uhaba wa vyumba 2 vya madarasa ambavyo wananchi wameshaandaa tofali na mchanga .
Pia Mwl.Kimaro amesema ushiriki wa wananchi wa Migandini katika maswala ya maendeleo ni wa kuigwa ambapo ametoa wito kwa uongozi wa shule kutunza madawati hayo.
Naye , Afisa elimu Kata Mwl. Juma Msangi amepongeza uongozi wa kijiji cha Migandini na kuhaidi kuendelea kushirikiana na wananchi wa Kata hiyo kuhakikisha wanainua taaluma .
Kulia ni Mwl.Exaud Kimaro akipokea Dawati toka kwa Mhe.diwani wa Kata ya Maroroni na Mwenyekiyi wa kijiji cha Migangini .
Mwl.Kimaro ambaye amemwakilisha mkurugenzi Wa halmashauri ya Meru akifanya makabidhiano ya madawati kwa uongozi wa shule.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mikandini wakifurahia madawati yaliyotolewa na uongozi wa Kijiji .
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa