Maadhimisho ya siku ya Afya na Lishe kwa Mkoa wa Arusha yameadhimishwa leo katika Hospitali ya Wilaya ya Halmashauri ya Meru yaliyoambatana na huduma mbalimbali za Afya kama upimaji wa hali ya lishe, ulinganisho wa Urefu na Uzito pamoja na kutoa elimu ya vyakula ya Afya na lishe.
Kwa niaba Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John VK. Mongella, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt. Charles Rashid Mkombachepa ameeleza kuwa dhumuni la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa katika jamii yetu kuhusu umuhimu wa lishe bora wa vijana.
" Lishe bora kwa vijana balehe ni muhimu kwa kipindi cha miaka 10 -19 kwani ni fursa adhimu ya ukuaji na maendeleo ya binadamu baada ya siku elfu moja za mwanzo wa maisha ya mtoto." Alisema Mkombachepa.
Aidha, ameeleza kuwa vijana balehe wana umuhimu wa kuzingatia lishe kwani ndio msingi wa maendeleo ya binadamu na ya Nchi.
Pia, ameeleza kuwa makadirio ya kidunia yanaonyesha kuna vijana Milion 1.2 wenye umri wa miaka 10-19 ambayo inaongezeka kwa kasi kubwa. Kwa Nchi ya Tanzania Vijana balehe wanakadiriwa kuwa robo ya watu wote kwa ujumla.
Mganga Mkuu H/Wilaya ya Meru Dkt. Evarist Chiweka ameeleza kuwa Afya bora ni muhimu kwa nguvu kazi ya Taifa. Pia alieleza madhara ya utapiamlo kwa wanawake na watoto wadogo ambao ndio wahanga wakubwa ambapo ameeleza utapiamlo unasababisha vifo kwa watoto wakati wa kujifungua, Kuzaa mtoto mwenye uzito pungufu na Kuzaa Mtoto ambaye hajafikisha muda wake(Njiti).
Iren Clement Makundi ni mwanafunzi kutoka chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, amefurahi kushiriki katika maadhimisho hayo kwani amejifunza umuhimu wa lishe bora kwa vijana balehe.
" Nimeokolewa na elimu finyu iliyokuwepo katika kichwa changu kwani leo nimeelewa umuhimu wa lishe bora kwa kijana hasa wakati wa kupevuka" Alisema Iren.
Ikumbukwe kuwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 Sura ya 3 Ibara ya 81, imeeleza kuwa huduma za Afya ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora ili kuwawezesha kushiriki katika shughuli za maendeleo ya Nchi.
Siku ya Afya na Lishe kitaifa imefanyika Mkoani Pwani. Kauli Mbiu ya mwaka 2023 ni " Lishe bora kwa Vijana balehe ni chachu ya mafanikio yao"
Dkt. Charles Rashid Mkombachepa akieleza dhumuni la maadhimisho ya siku ya lishe.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa