Na . Annamaria Makweba
Maafisa wa Serikali wapatao idadi ya 50 katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru wamepatiwa Mafunzo ya Usimamizi wa Miradi ya TASAF awamu ya III inayotekelezwa katika Halmashauri zote nchini Tanzania.
Mafunzo hayo yamefanyika leo tarehe 27 Agosti 2024 katika ukumbi wa Taasisi ya "The Foundation For Tomorrow(TFFT) na kufunguliwa na Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwl. Zainabu J. Makwinya.
Katika Ufunguzi wake, Mkurugenzi Makwinya amewataka Maafisa hao kusikiliza kwa makini na kuelewa kile wanachotakiwa kwenda kufanya ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri kwa miradi itakayoibuliwa na wananchi na siyo kwenda kuwaibulia miradi ya kutekeleza.
"Serikali inatoa mafunzo haya ili muende kuzisaidia jamii katika kuibua Miradi na siyo nyinyi kuwaibulia miradi kwani kwa kufanya hivyo jamii haitakuwa na umiliki wa miradi yao, hivyo lengo kuu ni nyinyi kwenda kuwasimamia ili waibue miradi ambayo kweli itakwenda kutatua changamoto zao.
Mratibu wa TASAF kutoka Makao Makuu Dodoma Bi. Godliver Mvanda ameeleza kuwa lengo la Mafunzo hayo ni kuwapitisha maafisa hao katika miongozo na kuteua wawezeshaji wanaofahamu mambo yanayohitaji utaalamu ili kuwezesha miradi hiyo kutekelezwa kwa ufanisi unaotakiwa.
Aidha, Bi. Mvanda ameeleza kuwa mpango huu umeandaliwa kwa malengo ya kumwezesha Mlengwa wa TASAF kushiriki katika kuibua miradi lakini pia kushiriki kufanya kazi ambazo zitamwingizia kipato ndani ya siku 60 kwa mwaka watakaofanya kazi hizo kwenye maeneo yao.
Kwa niaba ya Maafisa walioshiriki mafunzo hayo, Afisa Mifugo Merry Kiondo ametoa shukrani kwa Serikali kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo hayo lakini pia ameahidi kuzingatia maelekezo yote yaliyotolewa mafunzo hayo.
Maafisa walioshiriki katika Mafunzo hayo ni pamoja na Maafisa wa Mifugo, Kilimo, Wachumi, Maendeleo ya Jamii, Mazingira, Afya, Elimu Kata, Misitu na Maliasili, Uvuvi, Wahandisi na Umwagiliaji.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa