Kambi ya Madaktari Bingwa wa MAMA SAMIA MENTORSHIP PROGRAM wamefika
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru na kukutana na Mhe. Amir Mkalipa pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Meru na kukutana na Mwl. Zainabu J. Makwinya kwa lengo la kuonana na viongozi hao na kutoa mwanga wa namna watakavyofanya kazi ya kutoa huduma ya Afya katika Hospitali ya Wilaya ya Meru.
Madaktari hao wamewasili katika Hospitali ya Wilaya ya Meru Tarehe 21 Oktoba 2024 na watafanya kazi hadi tarehe 26, Oktoba 2024 kwa kutoa huduma za afya kwa jamii.
Mkuu wa Divisheni ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Evarist Chiweka ameeleza kuwa Madaktari Bingwa Saba wamefika kwenye kambi hiyo akiwemo daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, mfumo wa mkojo na upasuaji, Daktari bingwa wa Kinywa na Meno, Magonjwa ya akina mama na wanawake, Mtaalam wa Usingizi na gazi na Daktari bingwa wa watoto.
Chiweka ameeleza kuwa madaktari hao watatoa huduma kwa njia ya kliniki maalum na wagonjwa watapata fursa ya kupata ushauri na matibabu kutoka kwa madaktari bingwa kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Hospitali ya Wilaya Meru.
Aidha, ameeleza kuwa katika Kambi hiyo madaktari watafanya tathmini za afya, upasuaji wa dharura, na wanatoa elimu juu ya afya ya jamii. Walengwa ni wakazi wa Wilaya ya Meru na maeneo jirani, ambao wana changamoto za kupata huduma bora za afya.
Pia, ameeleza kuwa Huduma zinatolewa kwa ushirikiano na Wizara ya Afya na lengo ikiwa ni kuboresha upatikanaji wa huduma za afya za kibingwa kwa wananchi na hii ni hatua muhimu katika kuboresha afya ya jamii na kupunguza wingi wa wagonjwa kufuata huduma hizi kwenye Hospital za Rufaa.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa