Ili Uchumi wa Taifa uweze kukua Serikali inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na madereva wa Serikali katika kukuza uchumi huo katika Taifa letu.
Hayo yameelezwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa katika ufunguzi wa Kongamano la tatu la Madereva wa Serikali, linalofanyika katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Mkoani Arusha (AICC) Agosti 20, 2024.
Mhe. Majaliwa ameeleza kuwa Kada ya udereva ni muhimu kwa Serikali kutokana na huduma wanayoitoa kwa viongozi na Maafisa wa Serikali, ni kada ambayo inachochea maendeleo ya Taifa la Tanzania ikiwa inagusa jamii moja kwa moja.
"Madereva wa Serikali niwasisitize kufanya kazi kwa uadilifu, kusimamia maadili ya kazi kwa kuzingatia mahusiano mazuri kazini, Pia kuwa na nidhamu kazini ni suala la msingi sana, heshimuni alama za barabarani kwa kuzingatia usalama kwani unaanza na wewe, lindeni usalama wa abiria na waenda kwa miguu pamoja na usalama wa vifaa vinavyotumika"Amesema Waziri Mkuu
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu, ameeleza kuwa, Serikali itaendelea kuboresha miundo ya kiutumishi kwa madereva ili kuboresha maslahi yao, huku ikiwa imefanya mapitio ya miundo hiyo na kufanikiwa kubadilisha miundo ya madereva 1,600 pamoja na kutoa vibali vya ajira mpya, jambo ambalo limechangia idadi ya madereva kuongezeka.
Ameongeza kuwa, Kongamano hilo likatoe hamasa ya madereva kwenda kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia taratibu maadili ya udereva, kanuni, taratibu za utumishi wa Umma pamoja na miongozo ya Serikali, hali itakayoipa heshima kada ya udereva kuwa kama kada nyingine.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu, amefurahishwa na kauli mbiu ya Dereva Jitambue, Timiza Wajibu wako, Usalama Barabarani Unaanza na wewe" ambayo imebeba ujumbe muhimu na wa kipekee hasa kwa madereva na maslahi ya Taifa, kwa kutambua na kufahamu majukumu yao, dhamana ya kuwahudumia viongozi na wananchi na umuhimu wa kutekeleza majukumu na kuzingatia sheria na usalama wa barabarani.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa