Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Ndg. Emmanuel Mkongo amepiga marufuku Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule, Watendaji Kata na Vijiji kuwarudisha nyumbani Wanafunzi ambao Wazazi wao hawajatoa michango ya Chakula na Katarasi ambayo wamekubaliana kwenye Vikao Kamati za Shule,Bodi za Shule, Halmashauri za Vijiji na Mikutano Mikuu.
Katazo hilo, ni baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya Wananchi na Wazazi kulalamikia vitendo vya Wanafunzi kurejeshwa majumbani kutokana na wazazi wao kutokutoa michango .
Mkongo, amesema Halmashauri hiyo haitasita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu Walimu au Watendaji watakaohusika kuwarudisha nyumbani Wanafunzi kwa sababu za michango kwani kufanya hivyo ni kinyume na maelekezo ya Waraka wa Elimu Na. 3 wa mwaka 2016.
Aidha, Mkongo ametoa agizo hilo wakati wa Mkutano na Waheshimiwa Madiwani wa Kata ya Mbuguni na Shambarai Burka, Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji, Wajumbe wa Halmashauri za Vijiji, Watendaji wa Kata na Vijiji, Walimu na Waratibu Elimu wa Kata hizo uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Tarafa ya Mbuguni.
Ikumbukwe kuwa Serikali imekuwa ikitoa fedha kwaajili ya utoaji wa Elimu Bila Malipo katika shule za Sekondari na Msingi katika Halmashauri ya Meru.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa