MASWALI YA PAPO KWA PAPO KWA MHE. MWENYEKITI WA HALMASHAURI NA MKURUGENZI MTENDAJI WA HALMASHAURI.
Imewekwa: March 14th, 2024
Mkutano wa Baraza la Halmashauri kwa siku ya Pili uliotanguliwa na maswali ya Papo kwa Papo kwa Mheshimiwa Mwenyekiti wa Halmashauri na Mkurugenzi Mtendaji.
Wajumbe wa Mkutano na Waheshimiwa Madiwani wa Kata wameuliza maswali ya papo kwa papo kwa Mhe. Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na kupatiwa ufafanuzi wa maswali waliyouliza hii ni kwa Mujibu wa Kanuni ya 24 ya kanuni za kudumu za Halmashauri ya Wilaya ya Meru za mwaka 2014.
Kati ya maswali yaliyoulizwa ni pamoja na uharibifu wa maeneo unaosababishwa na mmea unaoitwa Gugu karoti, unaua majani yote kwenye eneo ambalo Gugu karoti hilo limeota na kusambaa.
Mkurugenzi Mtendaji Mwl. Zainabu J. Makwinya ametoa ufafanuzi kuhusu Gugu karoti na kueleza kuwa mmea huo siyo wa asili lakini una zaidi ya miaka 5 hapa Tanzania na tayari elimu ilishatolea juu ya madhara ya mmea huo kwa binadamu na mifugo. Pia ameeleza kuwa Gugu karoti hilo ni sawa na magugu mengine yanayochafua mazingira hivyo aliwataka viongozi kwenye maeneo yao kwa kushirikiana na Watendaji wa Kata na Vijiji kusimamia zoezi la kung'oa na kuyachoma moto sambamba na kufanya usafi wa mazingira katika maeneo ya makazi na mashambani.
Aidha, Wenyeviti wa Kamati za kudumu za Halmashauri wamewasilisha taarifa za Kamati zao na kutolea ufananuzi kwenye maeneo ambayo yamehitaji ufafanuzi.
Kamati hizo ni Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango, Kamati ya Elimu, Afya na Maji, Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira pamoja na Kamati ya Mpango wa kudhibiti UKIMWI.