MERU DC IMEFANYA KIKAO CHA KAMATI YA AFYA YA MSINGI
Imewekwa: November 10th, 2023
Halmashauri ya Meru imefanya kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) kwa ajili ya kutambulisha mpango wa uboreshaji wa afya ya mazingira na maji kwa mfumo wa Pay for Result).
Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Katibu Tawala Wilaya hiyo, Joseph Mabiti amefungua kikao hicho ambapo wadau mbalimbali kuanzia ngazi ya chini wanaopitiwa na mradi huo kama Watendaji wa Vijiji na Kata, Wenyeviti wa Vijiji, Wahe. Madiwani na Wataalam wa Halmashauri wameshiriki ili kujadiliana namna bora ya utekelezaji wa Mradi huo.
Katika Uwasilishaji wa taarifa ya Mpango huo Afisa Afya Wilaya Debora James Masaka ameeleza kuwa, mpango huo utatekelezwa katika vituo vya kutolea huduma za Afya, shule za msingi na katika vijiji. Lengo la mpango huo ni kuondokana na magonjwa ya kuambukiza pamoja upatikanaji wa maji safi.
Aidha, Afisa Afya alieleza kuwa vituo vilivyoteuliwa kwa ajili ya mradi ni kituo cha Afya Mareu, Zahanati ya Mulala, Zahanati ya Kwa Ugoro na Zahanati ya Maji ya Chai na Fedha zilizopokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi huo ni shilingi Milioni 238,848,519.12
Kwa upande wa Afisa Elimu Watu wazima ambaye ni mratibu wa Mradi wa SWASH Mariamu Omari Fyeku ameeleza kuwa shule zilizopata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu ni Shule ya Msingi Mavinuni na Shule ya Msingi Leguruki ambapo jumla ya Fedha ni shilingi Milioni 92,429,630.06
Hata hivyo, kutokana na Maelekezo kutoka OR- TAMISEMI katika utekelezaji wa mradi, watakaofanya vizuri wataiwezesha Halmashauri kupewa zawadi( Bonus) ya Fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika maeneo mengine.
Vilevile, Katibu Tawala Arumeru amesisitiza Viongozi wanaopitiwa na mradi huo, hasa Waheshimiwa Madiwani wakishirikiana na Watendaji wa Kata kwenye vikao vya maendeleo ya Kata (WDC) Watoe elimu kwa wananchi na kusimamia miradi hiyo ili iweze kukamika kwa viwango vinavyotakiwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Jeremia Kishili amesisitiza Wataalamu kuhakikisha wanasimamia Hatua zote za utekelezaji wa Mradi huo ili ijengwe kwa ubora unaotakiwa na kuleta tija kwa wananchi.