Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango ametoa wito kwa viongozi wa Dini ,Viongozi wa kijamii na wadau wengine katika sekta ya afya kutoa elimu kwa jamii ikiwa ni kuchukua tahadhari juu ya Ugonjwa wa Ebola ambao mlipuko wa ugonjwa huo umeripotiwa nchi Jirani ya Uganda.
Mhe.Ruyango amesema hayo wakati wa Kikao cha kamati ya Afya ya Msingi (PHC) ngazi ya Wilaya Halmashauri ya Wilaya ya Meru ambapo amesema Kutokana na muingiliano kati ya nchi na nchi ,hatuna budi kuchukua tahadhari kwani kuna uwezekano wa ugonjwa huo kuenea .
Akiwasilisha Mada ya Ugonjwa wa Ebola, Dkt.Emmanuel Kinayi amesema Ugonjwa wa Ebola hauna tiba maalum wala chanjo kwani Mgonjwa hupewa tiba saidizi kulingana na dalili alizonazo , kama vile Tiba ya kushusha homa na maumivu, Kuongezewa damu na maji mwilini, Tiba lishe.
Dkt. Kinayi amesema ugonjwa wa Ebola unasababishwa na virusi vya Ebola ambavyo hubebwa na wanyama kama vile Nyani,Sokwe,Gorilla,Kima ,Popo ,Swala swala ambapo husambazwa kutoka kwa wanyama hao kwenda kwa binadamu kwa kula nyama,mizoga au kuwagusa.
Vilevile Dkt.Kinayi amesema ugonjwa wa Ebola huenezwa kupitia sehemu za wazi za mwili kama vile pua, masikio na macho ambapo humuathiri binadamu na wanyawa endapo vimelea vitaingia katika mzunguko wa damu .
Mkuu wa Idara ya Afya,Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt.Focus Maneno ametoa wito kwa jamii kujikinga na ugonjwa wa Ebola kwa kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono au kukumbatiana, kutokugusa damu , matapishi , mkojo ,kinyesi , kamasi , mate , machozi na maji mengine yanayotoka mwilini mwa mtu mwenye dalili za ugonjwa huu, kutokugusa au kuosha maiti ya mtu aliyekufa akiwa na dalili za Ebola, kuepuka kutumia nguo , shuka , blanketi , kitanda na godoro za mtu aliyeambukizwa ugonjwa huu, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni mara kwa mara,kuepuka kugusa wanyama kama vile popo , nyani , sokwe , tumbili na swala au mizoa ya wanyama
Dkt.Maneno amesema endapo mtu atakuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola ambazo huonekana kati ya siku 2 hadi 21 baada ya mtu kupata maambukizi kutoa taatifa mapema kwa uongozi ambapo ametaja dalili hizo kuwa ni pamoja kuwa na homa kali ya ghafla,maumivu ya kichwa,maumivu ya mwili , misuli na viungo,
Kuharisha (kunakoweza kuambatana na damu),Kutapika (kunakoweza kuambatana na damu),Vipele mwilini,
Kuvia damu chini ya ngozi au kutokwa na damu puani , mdomoni , machoni na masikioni.
Aidha amesisitiza kuwa hadi sasa hakuna mgonjwa wa Ebola aliyegundulika na hivyo ameomba wadau wote kushirikiana na sekta/Idara ya Afya ili kufanya maandalizi muhimu ya kukabiliana na mlipuko wa magonjwa ikiwemo Ebola.
*UGONJWA WA EBOLA HAINA TIBA ,TUJIKINGE KWA KUCHUKUA TAHADHARI*
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango akizungumza wakati wa kikao.
Viongozi wakisikiliza taarifa ya ugonjwa wa Ebola.
Viongozi wa Dini ,Viongozi wa kijamii ,na wataalum wakati wa kikao
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa