Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Wilayani Arumeru imezindua rasmi kampeni ya siku nne kuanzia tarehe 18 hadi 21 Mei 2022 ya chanjo ya matone ya polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5 .
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwl.Zainabu Makwinya amesema kampeni hiyo ya utoaji chanjo ya polio itafanyika nyumba kwa nyumba na kuhimiza kila mzazi/mlezi kuhakikisha watoto wanapata chanjo hiyo muhimu .
Aidha, Mwl.Makwinya amesema kampeni ya chanjo ya Polio ni ya Kitaifa na inalenga kuongeza kinga mwili kwa watoto chini ya umri wa miaka 5 ili kuzuia maambukizi ya kirusi cha Polio, ikizingatiwa kirusi hicho kiliripotiwa kuwepo nchi jirani ya Malawi.
Aidha Mwl.Makwinya amewashukuru wadau waliochangia kufanikisha kampeni hiyo kwa kutoa magari na amewaagiza wataalum kuimarisha usimamizi wa utoaji huduma za chanjo kwa kipindi chote cha kampeni hiyo.
Mganga Mkuu Wilaya Dkt.Maneno Focus amesema chanjo ya Polio ni muhimu sana kwani ugonjwa wa Polio unaosababishwa na kirusi ambacho huambukizwa kwa kula au kunywa kitu kilichochafuliwa na kinyesi chenye vimelea hauna tiba.
Miongoni mwa wazazi walio hudhuria uzinduzi huo wamehimiza kila mzazi kuona umuhimu wa chanjo hiyo, Izack Pallangyo ametoa wito kwa wazazi wa kiume kuwa mstari wa mbele kuhakikisha watoto wanapata chanjo hiyo "kinga ni bora ikizingatiwa, Polio haina tiba"amehimiza Ndg.Pallangyo
Naye Zenice Kiriho ambaye ni mama wa mtoto wa kwanza kupewa chanjo wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ameishukuru Serikali kuhakikisha chanjo ya polio inapatikana na kurahisisha utoaji wake ambapo mbali na kutolewa kwenye vituo vya tiba itatolewa nyumba kwa nyumba.
Uzinduzi huo wa Kampeni ya Chanjo ya Polio katika Halmadhauri ya Wilaya ya Meru umefanyika katika kituo cha Afya Usa-River ambayo inalenga kuwafikia watoto 39,649 katika halmashauri ya wilaya ya Meru.
_Muhimu Mtoto asiyepata chanjo ni hatari kwa maisha yake na kwa jamii inayomzunguka mwani anaweza kuambukizwa au kuwaambukiza wengine._
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa