Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Wilayani Arumeru yazindua miongozo mitatu ya usimamizi wa elimu nchini, iliyotolewa na serikali kupitia wizara ya elimu inayolenga kuimarisha utoaji wa elimu bora. miongozo hiyo ni Mkakati wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimumsingi ,Changamoto katika uboreshaji wa elimu ya msingi na Uteuzi wa Viongozi wa Elimu katika mamlaka za serikali za mitaa ,
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru wakati wa hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha Elimu Maalum Patandi, Bw Said Mzava ambaye pia ni Afisa Tarafa, tarafa ya Poli amesema Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuongeza uwekezaji katika sekta za Elimumsingi na Sekondari ili kuhakikisha watoto wote wa kitanzania wakiwemo wenye mahitaji maalum wanapata elimu bora katika mazingira rafiki.
Mzava amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu imeandaa miongozo hiyo ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimumsingi na Sekondari ,kutatua changamoto katika uboreshaji wa elimu pamoja na kuwa na viongozi watakaoleta tija kwenye sekta ya Elimu ambapo ametoa wito kwa Walimu kutekeleza wajibu wao wa kufundisha kwa weledi na uzalendo mkubwa ili kuwasaidia walengwa ambao ni wanafunzi
Vilevile Mzava amehimiza kila mhusika kuzingatia miongozo hiyo ambayo utekelezaji wake umeanza ikiwa ni pamoja na uandikishaji wa darasa la awali na la kwanza unaoanza mwezi Oktoba na kukamilika kabla ya kufunguliwa shule Januari 2023.
Mwl.Marcus Nazi ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Meru amesema Serikali imetumia gharama kuandaa miongozo hiyo yenye tija kwa wanafunzi wakiwemo wa Darasa la Kwanza na la pili kumudu stadi za KKK (kusoma,kuhesabu na kuandika) hivyo walimu hawana budi kuitekeleza miongozo hiyo.
Kwa upande wake Emmy Mfuru Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri hiyo amesema Miongozo hiyo inatija kubwa kwenye kuboresha Elimu kwa kubaini changamoto pamoja na kutoa utatuzi wa changamoto hizo .
Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari wameishukuru Serikali kwa kuanda miongozo hiyo yenye mikakati mahususi ya kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata elimu bora "Tunaishukuru Serikali kwani hata sisi wenye mahitaji maalumu ni wanufaika wa miongozo hii"amesema Hollyness mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya Sekondari Patandi Maalum
Aidha, hafla hiyo ya uzinduzi wa Miongozo ya elimu imewajumuisha Maafisa toka Idara za Elimu Msingi na Sekondari,Maafisa Elimu Kata ,Watendaji wa Kata ,Wanafunzi wa Shule za msingi na Sekondari na wadau wengine wa elimu akiwemo Mkuu wa Chuo Patandi, Katibu CWT Wilaya ya Arumeru, Mthibiti Ubora wa Shule,Katibu TSC ambapo Maafisa elimu Kata na Watendaji Kata wamekabidhiwa miongozo hiyo.
✍️ *Awamu ya Sita na Uimarishaji,Uboreshaji Sekta ya Elimu*
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa