MKURUGENZI MERU DC AKABIDHIWA TUZO YA UTENDAJI MZURI KATIKA SEKTA YA MIFUGO, KILIMO NA USHIRIKA
Imewekwa: November 16th, 2023
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwl. Zainabu J. Makwinya amekabidhiwa tuzo 3 za Sekta ya Mifugo, Kilimo na Ushirika.
Akikabidhiwa tuzo hizo ofisini kwake na Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Aman Sanga pamoja na Afisa Kilimo Bw. Ridhiwani Kombo mara baada ya kushiriki katika kikao kazi cha Wataalam wa sekta za Uchumi Mkoa wa Arusha -Ngorongoro kilichofanyika hivi karibuni.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru imepata tuzo ya Mshindi wa Kwanza Kimkoa kwa utendaji mzuri katika Sekta ya Mifugo. Lakini pia, imepata tuzo ya utendaji mzuri wa shughuli za Kilimo pamoja na Ushirika.
Aidha, katika kikao hicho cha ugawaji wa tuzo watumishi wanne wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru wamepata vyeti vya pongezi kwa utendaji mzuri katika sekta mbalimbali.
Watumishi hao ni Dkt. Charles Msigwa wa sekta ya Mifugo ameshika nafasi ya kwanza Kimkoa, Bw. Ridhiwani Kombo wa sekta ya Kilimo ameshika nafasi ya pili Kimkoa. Bw. Mussa Mkumbwa wa sekta ya Ushirika ameshika nafasi ya kwanza Kimkoa na Bi. Annastazia Mahoo wa sekta hiyo ya Ushirika ameshika nafasi ya pili Kimkoa.
Ugawaji wa tuzo hizo umefanyika katika kikao cha Tathmini ya utendaji kazi wa wataalam wa sekta za Kilimo,Mifugo,Maliasili, Hifadhi ya Mazingira na Ushirika toka Halmashauri pamoja na wadau wa taasisi za Kiserikali na zisizo za Kiserikali.
Lengo la Tuzo hizo ni kuboresha utendaji kazi kupitia upatikanaji wa taarifa na takwimu sahihi za kisekta na kuboresha mahusiano ya kazi katika sekta hizo.