Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Kaganda ametoa wito kwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Wilayani humo kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo ili miradi hiyo kuwa na tija .
Mhe.Kaganda amesema hayo wakati wa Mkutano wa baraza la Halmashauri hiyo, ambapo amesema Serikali ya awamu ya Sita ikiongozwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka jitihada kubwa katika kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuboresha miundombinu katika sekta za Elimu, Afya,Maji nk.
Mhe.Kaganda amesisitiza Madiwani hawana budi kusimamia maendeleo hayo ya Serikali kwa karibu ambapo amebainisha hivi karibuni Serikali ya awamu ya sita imetoa fedha Milioni 961.5 za Mradi wa BOOST kwa ajili ya Ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika shule za msingi na zaidi ya Milioni 615 imetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kidato cha 5 na 6 shule ya Sekondari Makiba.
Aidha ,Mhe.Kaganda amesema sambamba na usimamuzi wa miradi, Madiwani wanapaswa kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo katika ofisi za kiijiji na Kata ikiwa ni pamoja na kusomewa taarifa za mapato na matumizi katika mikutano ya hadhara kwa wakati.
Mheshimiwa Kaganda ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Meru kupata hati Safi kwa mwaka wa Fedha 2021/2022 ambapo amewataka waheshimiwa madiwani na wataalamu kuendelea kushirikiana kuiletea Halmashauri hiyo maendeleo sambamba.
Mwisho, Mhe Kaganda amewataka Waheshimiwa Madiwani na Wataalamu kuweka nguvu katika kujibu hoja za Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) kwa wakati na usahihi.
Kwa upande wao madiwani wa Halmashauri hiyo wamewahakikishia wananchi wataisimamia vyema Halmashauri hiyo kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na cha kesho " sisi Meru tunashirikiana vyema na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na viongozi wengine kuhakikisha tunafanya vizuri na kuwaletea wananchi maendeleo" amesema Mhe.Felista Nanyaro Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa