Afisa Lishe Halmashauri ya Wilaya ya Meru Bi. Asia Ijumaa amewataka wataalam kuendelea kutoa elimu kwa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru kuhakikisha wanafunzi shuleni wanapata Chakula bora na chenye virutubisho ili kuwasaidia watoto kuwa na lishe bora.
Afisa Lishe amesema hayo katika kikao cha Kamati ya Lishe kilichofanyika Leo tarehe 18 Oktoba, 2024 cha kujadili taarifa za Lishe kwa kipindi cha robo ya Kwanza Julai - Septemba 2024 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Afisa Lishe ameeleza kuwa mlo kamili ni ule unaozingatia Makundi 6 ya vyakula kwa siku, ambapo Makundi hayo ni kundi la Nafaka, Mizizi na Ndizi, Mbogamboga, Matunda, Kundi la asili ya wanyama, Jamii ya Mikunde pamoja na Mafuta yanayotokana na mimea.
Katika Kikao hicho, Divisheni za Elimu Msingi na Sekondari, Divisheni ya Afya, kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Maendeleo ya Jamii wamewasilisha taarifa na kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maeneo yao hasa katika Divisheni ya Kilimo kuhusu mazao ya Mbogamboga na matumizi ya viwatilifu.
Afisa Kilimo Ally Isimbula ameeleza kuwa changamoto hiyo wameshaanza kuifanyia kazi na wamejipanga kutoa elimu kwa wakulima ili kuzingatia matumizi sahihi ya viwatilifu na kulinda afya za walaji wa mbogamboga kwa wananchi wa Meru na Maeneo mengine.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwl. Zainabu Makwinya, Afisa Maendeleo ya Jamii Bi. Flora Msilu amewataka wataalam wanaohusika na masuala ya lishe wahakikishe wanashikiri katika vikao vya WDC na vikao vya wazazi ili kuendelea kutoa elimu kwa wazazi na jamii kuhusu masuala ya Lishe.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa