Msimamizi wa Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa Mwaka 2024 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwl. Zainabu J. Makwinya amefanya zoezi la kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura la uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa katika Kituo cha Nganana kijiji cha Nambala, Kata ya Kikwe katika Halmashauri hiyo.
Aidha, Mwl. Zainabu ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura na kuwataka watumishi wanaoishi maeneo mengine tofauti na vituo vyao vya Kazi kwenda kujiandikisha kwenye vituo vyao mahali wanapoishi.
Hata hivyo, Makwinya ameeleza kuwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Meru kuna vituo vya kujiandikisha na kupiga kura 338 na zoezi hili linaanza saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni. Pia, ameeleza wahusika ni wale walitimiza umri wa miaka 18 na kuendelea na kwa wale wanaogombea nafasi ya uongozi ni miaka 21 na kuendelea.
Katika Zoezi hilo Mwananchi wa Kijiji cha Nambala Mathew Mtinange ameeleza kuwa zoezi hilo linafanyika kwa muda mfupi na ameshukuru amekuta waandikishaji wapo kituoni.
" Zoezi ni Zuri nimejiandikisha kwa wakati na sijatumia muda mrefu hivyo niwashauri wananchi wenzangu kujitokeza kwani ndio njia pekee ya kupata viongozi tunaowataka. " Amesema Mathew.
Kiongozi wa Kanisa la IEC la Bishop Eliudi Issangya Kata ya Kikwe kijiji cha Nambala Mch. Simon Kaaya ameeleza kuwa zoezi hilo ni zuri na litawafanya kuchagua viongozi waliochaguliwa na Mungu na wanadamu pia.
"Uchaguzi wa Viongozi ulianzia kwenye Bibilia wakati wa Mussa hivyo ni wajibu wetu kujiandikisha ili kuweza kuchagua viongozi watakaotuongoza" amesema Mch. Kaaya.
Kwa upande wa Vijana, Rajabu Ramadhani ambaye naye amejitokeza kujiandikisha amewataka vijana kuwa wazalendo na kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la Wapiga Kura.
"Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi"
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa