Wanafunzi 80 wa kidato cha Kwanza wapangwa kuanza masomo katika shule mpya ya Sekondari ya Kiwawa .
Wanafunzi hao 80 wameongeza idadi ya wanafunzi waliopangwa kwa awamu ya pili kufikia 176.
Ikumbukwe kuwa, katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru idadi ya wanafunzi 6,851 walichaguliwa kujiunga kidato cha kwanza ambapo kati yao 5,216 walipangwa kwa awamu ya kwanza na 1,635 hawakupangwa kutokana na uhitaji wa vyumba vya madarasa .
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe.Jeremiah Kishili pamoja na Mkurugenzi Mtendaji Ndg. Emmanuel Mkongo waliitembelea shule hiyo kukagua miundombinu ambapo walitoa maelekezo kwa Kamati ya ujenzi ya shule hiyo kukamilisha miundombinu ya maji ili wanafunzi waweze kuanza masomo mapema.
"Tumeridhishwa na ujenzi katika shule ya Sekondari Kiwawa yenye madarasa 4, Viti na meza 100 , hivyo tumewapanga wanafunzi 80 kuanza masomo siku ya Jumatatu" ameeleza Mkongo.
Mkongo ameongeza kuwa Shule ya Sekondari Kiwawa ni ya pili kupangiwa wanafunzi ikitanguliwa na Shule ya Sekondari Nkoarisambu iliyopangiwa wanafunzi 96 baada ya kukamilisha vyumba 2 vya madarasa vilivyokua vinahitajika.
Mkongo amehitimisha kwa kutoa wito kwa Waheshimiwa Madiwani ,Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji, Watendaji wa Kata na Vijiji kusimamia ukamilishaji wa madarasa hayo kabla ya tarehe 28 Febriari 2021 kama Serikali ilivyoelekeza.
Katika kuhakikisha vyumba vya madarasa vinakamilika, Halmashauri ya Wilaya Meru kupitia fedha za mapato yake ya ndani (Own Source) imetumia zaidi ya Shilingi Milioni 160 kununua vifaa vya ujenzi ambavyo ni Bati 1860 zilizogharimu shilingi 48,259,004.51, Mbao shilingi 64,598,752.00 na Saruji mifuko 3325 iliyogharimu shilingi 48,212,500.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa