fungua hapa kupata video,☝️Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA Wilaya ya Arumeru imefanya Mkutano Mkuu wa nusu mwaka wa Pili kwa Vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya Jamii (CBWSOs) Wilaya ya Arumeru na kusikiliza changamoto mbalimbali za vyombo vya watumia maji.
Mkutano huo umefanyika leo katika ukumbi wa St. Carolus Tengeru na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali kama vile Waheshimiwa Madiwani,Watendaji wa Kata, Wataalamu wa Halmashauri, Maafisa Tarafa, Viongozi wa Dini, Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Wataalamu wa Bonde ( Pangani na Kati)Meneja wa Maabara ya Maji pamoja na viongozi wa Vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya jamii Arumeru.
Kati ya Changamoto zilizowasilishwa katika Mkutano huo ni uharibifu wa miundombinu, Taasisi kutolipa bili za maji, kupasuka kwa mabomba, baadhi ya viongozi kuhamasisha jamii isichangie huduma za maji, malipo ya uendeshaji wa miradi kuchelewa na kupelekea ufuatiliaji wa vyombo hivyo kuwa mgumu.
Meneja wa RUWASA Arumeru Mhandisi Shabib Waziri ameeleza kuwa Mkutano huo ndio Nuru kwa namna gani miradi au skimu za maji zitakavyoendeshwa na kusimamiwa ili kutoa Matunda.
" Hapa ndio sehemu sahihi ya kujadili changamoto zetu za vyombo vya watoa huduma za maji na sisi kama RUWASA tutoe changamoto zetu, tusisubiri afike kiongozi mkubwa ndio tuanze kutoa changamoto wakati tungeweza kuzifanyia kazi wenyewe" amesema Waziri.
Pia, ameeleza kuwa hawategemei ikitokea Ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo wakutane na malalamiko kuwa shule haina maji au Zahanati haina maji wakati maombi yao ya kuomba huduma hiyo hayakuwasilishwa RUWASA.
Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Kaganda, Afisa Tarafa ya Poli Ndg. Jiliki Milinga amewataka Viongozi mbalimbali walioshiriki katika Mkutano Mkuu wa Wilaya kwa vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya jamii kwenda kutoa elimu kwa wananchi umuhimu wa maji na kuchangia huduma ya maji ili vyanzo vya maji viweze kutunzwa na kutumika kwa vizazi vijavyo .
Milinga ameeleza kuwa adhma ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha tunamtua Mama Ndoo Kichwani na Serikali imeongeza fedha kutoka Bilioni 1 hadi Bilioni 6 ya utekelezaji wa miradi ya maji kuhakikisha adhma hiyo inatimia.
Kati ya Vyombo vya watumia maji viliyoshiriki Mkutano huo kwa Halmashauri ya Meru ni pamoja KIWANGO, MAKIMAKA, AMSHA, KIMASAKINA, MAKILENGA, NGUNGYESA na vingine.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa