Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Arumeru Bw.Deo Mtui amewaelimisha Watendaji wa Kata 53 na Watendaji wa Vijiji 187 kutoka kwenye Halmashauri mbili ya Arusha na Meru katika Wilaya ya Arumeru.
Elimu hiyo imetolewa katika Semina iliyoandaliwa na Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe.Emmanuela Kaganda tarehe 23.08.2023 na kuhudhuriwa na Kamati ya Usalama Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri hizo, Maafisa Tarafa 6 na Watendaji wa idara za Serikali.
Mkuu wa TAKUKURU Bw. Deo Mtui amewaelimisha Watendaji kuhusu maswala ya rushwa, sababu zake, athari zake, na kuwapitisha katika makosa ya rushwa lakini zaidi amewaelezea kuhusu maeneo yanayolalamikiwa kwa rushwa kwa Watendaji wa Kata na Vijiji na wajibu wa Watendaji wa Kata na Vijiji katika mapambano dhidi ya rushwa.
Aidha, Bw. Mtui amewataka Watendaji hao kuwa na tabia ya kusoma na kujadili taarifa za Mapato na Matumizi katika Mikutano yao Mikuu ya Vijiji kila baada ya miezi mitatu kwani ni takwa la kisheria na kutokufanya hivyo ni kosa la rushwa, ambapo wanakua wameenda kinyume cha sheria Na.7 ya Serikali za mitaa ya mwaka 1982 kif. cha 8, kipengele cha pili na kushindwa kutekeleza sheria hiyo inapelekea ukiukwaji wa moja kwa moja wa sheria Na.11/2007, sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kif. cha 31.
Vile vile, ameeleza kuwa Watendaji ambao watawasilisha/ wamekua wakiwasilisha taarifa za Mapato na Matumizi zenye upotoshaji kwa njia za kughushi wanakiuka kif. cha 22 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ambapo uchunguzi ukifanyika na kuthibitika pasipo na shaka ya kwamba, wamekiuka sheria hizo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa