TAKUKURU YATOA ZAWADI KWA WANAFUNZI WA VILABU VYA KUPINGA RUSHWA.
Imewekwa: February 15th, 2024
TAKUKURU Wilaya ya Arumeru imetoa Zawadi kwa wanafunzi wa Vilabu vya kupinga Rushwa kufuatia shindano la kuchora Katuni na Uandishi wa Insha zenye maudhui ya kuzuia, kuelimisha, kupinga na kupambana na Rushwa lililofanywa na shule za Sekondari za Halmashauri ya Arusha na Meru katika Wilaya ya Arumeru.
Zawadi hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Kaganda kwenye ukumbi uliopo kwenye ofisi ya jengo la Mkuu wa Wilaya hiyo.
Mhe. Kaganda ametoa pongezi nyingi kwa Wanafunzi walioshinda kwani wameonyesha uwezo wao mkubwa kwa kuifahamu rushwa na kuweza kuchora na kuandika Insha zinazoelezea mapambano ya kupinga Rushwa .
"Nimefurahishwa sana na kazi nzuri zilizofanywa na wanafunzi hawa, kwani wameelewa maudhui mbalimbali ya masuala ya utawala bora na kuhimiza Serikali za Vijiji kusoma na kujadili taarifa za Mapato na Matumizi, kukemea na kupambana na rushwa kwenye Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama barabarani, Utoaji haki ikiwemo Mahakama na Polisi" Alisema Kaganda.
Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Arumeru Deo Mtui ameeleza kuwa jumla ya shule za Sekondari 103 ziliandikiwa barua kushiriki, Shule 27 za Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na Meru zilishiriki kuimarisha vilabu vyao kwa kuandika insha na kuchora katuni zenye maudhui ya kuzuia, kuelimisha,kukemea na kupaambana na rushwa.
Aidha, amezitaja shule 4 kati ya 27 zilizoibuka kuwa washindi ambazo ni shule ya Sekondari Kikatiti na Maji ya Chai zilizopo Halmashauri ya Meru pamoja na Shule ya Sekondari Bangata na Olomitu zilizopo Halmashauri ya Arusha.
Kati ya Wanafunzi walioshiriki mashindano ya kuchora katuni na kuandika Insha ni Jovin Emmanuel Mgeni, Sedekia Evarest Longoare, Anitha Adam Siara, Reginald Timothy Makambu na Vicent Paul Urio. Ambapo waliandika insha tofauti kuhusu rushwa ya Ngono huathiri Utendaji kazi wa sekta mbalimbali, Wajibu wa Vijana katika mapambano dhidi ya rushwa pamoja na kuchora katuni yenye maudhui ya kukemea na kupambana na rushwa.
Wakurugenzi wa Halmashauri ya Arusha na Meru pamoja na Wakuu wa Idara za Elimu Sekondari wameishukuru TAKUKURU kwa kuanzisha mashindano ya vilabu vya kupinga rushwa Arumeru.