TUKUMBUSHANE MALEZI, MAKUZI NA MAENDELEO YA AWALI YA MTOTO
Imewekwa: December 4th, 2023
Na Annamaria Makweba,
Halmashauri ya Wilaya ya Meru imefanya kikao cha Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto (PJT- MMMAM) lengo ikiwa ni kukumbushana Malezi na Makuzi ya Mtoto tangu akiwa mwaka O .
Mwenyekiti wa Kikao hicho Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Blandina Nkini, ameelaza kuwa malezi ya mtoto yanaanzia tangu Mimba inatungwa hadi mtoto anapozaliwa.
" Mtoto anahitaji kupata malezi bora kutoka kwa baba na mama tangu mimba inapotungwa kwani mtoto anapokuwa katika tumbo la mama anauwezo wa kuanza kusikia kwenye wiki ya 16." Alisema Nkini
Aidha, Nkini amewataka kina baba kuwa sehemu ya malezi na kuacha tabia ya kuwa wafadhili kwa kutoa pesa za mahitaji ya watoto wao na kusahau jukumu la malezi na kumuachia mama peke yake.
Mkurugenzi wa Maasai Pastroralist Devote Initiatives ( MPDI) Arusha, Mohamed Nkīnde amesisitiza suala kuwaweka watoto karibu na kuwafanya kuwa marafiki ili wanapopata changamoto iwe rahisi kuwaeleza wazazi changamoto hizo.
" Mfanye mtoto kuwa rafiki yako wewe kama mzazi ili awe huru kuzungumza changamoto anazokutana nazo hata pale anapofanyiwa ukātili. " alisema Nkīnde.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Florah Msilu ameeleza kuwa Halmashauri hiyo imefanikiwa kuunda Mabaraza ya Watoto katika Kata Kata zote pamoja na Klabu za watoto ambazo pia zitasaidia masuala ya malezi na makuzi kwa watoto. Lakini pia umewekwa utaratibu kwa kushirikiana na kamati za shule ili wanapoitisha vikao waweze kukutana na wazazi na kutoa elimu hiyo.
Ikumbukwe kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Rais Dkt . Samia Suluhu Hassan inasimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 imeendelea kusimamia Sera ya Taifa ya Maendeleo ya mtoto, katika Sura ya 92 (b) moja ya Mafanikio yaliyopatikana ni kusimamia utoaji wa huduma ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali kwa watoto walio chini ya miaka mitano walio katika vituo vya kulelea watoto wadogo mchana vimeongezeka kutoka vituo 744 mwaka 2015 hadi vituo 1,538 mwaka 2020.