Leo tarehe 19 Oktoba 2024 Mkutano wa Baraza la Mwisho la Mamlaka ya Mji Mdogo Usariver umefanyika kwa ajili ya kupokea taarifa ya Utekelezaji kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba 2024 kwa mwaka wa Fedha 2024/2025 pamoja na Kuvunja Baraza la Mamlaka ambalo wajumbe wake ni Wenyeviti wa Vitongoji 9 baada ya kufikia Ukomo kwa kipindi cha miaka Mitano ya Uongozi wao.
Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mhe.Godson Majola Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Meru na Kuongozwa na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo Usariver ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mji Mwema Bw. Dalton G.Lema.
Mwenyekiti Dalton ametoa shukrani kwa wajumbe wote wa mamlaka kwa ushirikiano waliompa kwa kipindi chote akiwa Mwenyekiti wa Mamlaka, pia amewapongeza wataalam kwa kuwajibika katika utendaji wa kazi za kila siku.
Aidha, katika Kikao hicho Wataalamu mbalimbali wa Halmashauri wamewasilisha taarifa za utekelezaji kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba 2024 na Afisa Utumishi Mkuu Bi. Furahisha Magubila kwa niaba ya Afisa Mtendaji Wa Mamlaka ya Mji Mdogo amewasilisha taarifa ya Ukomo wa Viongozi hao kwa mujibu wa Kanuni ya 21 ya kanuni za Uchaguzi wa Wenyeviti wa Vitongoji katika Mamlaka ya Mji Mdogo, Tangazo la Serikali Na. 572 la mwaka 2024.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mhe. Jeremia Kishili ameshikiri Katika Mkutano huo, aidha amewapongeza viongozi hao kwa kazi nzuri walizozifanya kwa kipindi chote cha miaka Mitano na kuwataka kushiriki zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la wakaazi na uchaguzi . Pia kwa wale watakaowiwa kugombea nafasi za uongozi kwa mara nyingine wagombee pindi muda utakapofika.
"Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi"
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa