Witness Ayo ambaye ni mkazi wa Leguruki ameweka rekodi ya uzinduzi wa huduma ya upasuaji katika Kituo cha Afya Usa –River kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Meru baada ya kujifungua mtoto kwa kufanyiwa upasuaji kituoni hapo.
Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dkt. Nuruel Kitomari amesema zoezi hilo la upasuaji limeenda vizuri na kuishukuru Serikali kwa kutenga Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya uboreshaji wa Kituo hicho kwa kujenga majengo mapya likiwemo jengo la upasuaji.
Dkt. Kitomari amesema kuzinduliwa kwa huduma hiyo kutawapunguzia wananchi gharama kwa kuwa huduma hiyo ni bure katika vituo vya afya vya Serikali ukilingalinganisha na vituo vingine pia kupunguza msongamano katika Hospitali ya Wilaya. Aidha, uwepo wa Kituo hicho utasaidia mama wajawazito katika maeneo ya Usa River na maeneo jirani kupata huduma za uzazi hususani upasuaji kwa urahisi zaidi.
Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dkt.Focus Maneno amesema Serikali imelenga kuboresha huduma za afya ambapo upatikanaji wa dawa katika Halmashauri hiyo ni asilimia 98%, pia katika kuondoa vifo vitokanavyo na uzazi Serikali imesogeza huduma hizo karibu na wananchi ambapo huduma ya upasuaji kwa Mama wajawazito inapatikana katika vituo vya afya vitatu vya Halmashauri hiyo ambavyo ni Usa – River, Kituo cha Afya Mbuguni na Kituo cha afya Momela.
Akizungumza na Mwandishi wetu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Ndg. Emmanuel Mkongo amesema uboreshaji wa Sekta ya Afya ni kipaumbele cha Serikali ya awamu ya tano, Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018 ilitoa Shilingi milioni 500 kwaajili ya ujenzi na uboreshaji wa Kituo cha Afya Usa -River hususani ujenzi wa majengo mapya ambayo ni jengo la maabara, nyumba ya mtumishi, jengo la upasuaji, wodi ya mama na mtoto, chumba cha kuhifadhia maiti, kichomea taka pamoja na kufanya ukarabati wa majengo yaliyokuwepo ambayo ni Jengo la kuwahudumia wagonjwa wa nje (OPD), jengo la duka la dawa ambalo awali lilitumika kama kama jengo la Maabara, Jengo lenye pande mbili likitumika kama wodi ya wanawake na wanaume .
BAADHI YA PICHA.
Madaktari na wataalam wa afya wakati wa zoezi la upasuaji kituo cha Afya Usa - river.
Mashine ya dawa za usingizi katika chumba cha upasuaji kituo cha Afya Usa river.
Taa maalumu katika chumba cha upasuaji kituo cha Afya Usa river.
Chombo cha kutakasia vifaa vya upasuaji kituo cha Afya Usa river.
Kitanda maalumu cha kubeba Wagonjwa wa upasuaji katika kituo cha Afya Usa - River
Muonekano wa ndani wa jengo la upasuaji katika kituo cha Afya Usa - River.
Muonekano wa nje wa Jengo la upasuaji kituo cha Afya Usa -River.
Jengo la Wodi ya Mama na Mtoto katika kituo cha Afya Usa - River.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa