WAJAWAZITO WAPEWE ELIMU WAHUDHURIE KLINIKI MAPEMA - DC MKALIPA.
Imewekwa: December 27th, 2024
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Amir Mkalipa amewataka wataalamu wa Afya kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii ili kuhimiza kina mama wajawazito kuanza mapema kuhudhuria Kliniki na kujua hali zao ili kuondokana na vifo vinavyotokana na uzazi.
Mkalipa ameeleza hayo katika kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) cha Halmashauri ya Wilaya ya Meru cha kujadili taarifa kipindi cha Julai hadi Septemba 2024 kilichofanyika tarehe 27 Desemba 2024 katika Ukumbi wa shule ya Sekondari Muungano iliyopo Usariver.
" Hakikisheni elimu inatolewa kwa jamii na wazazi wote kuzingatia muda wa kuanza kliniki ili kujua hali zao za kiafya kabla ya kujifungua, wakati wa kujifunga na baada ya kujifungua kwani Vifo vingi ni kutokana na kutozingatia huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto." Amesema Mkalipa.
Aidha, ameeleza kuwa Halmashauri ya Meru iweke mikakati ya kuondoa vifo vya uzazi kutoka kifo 1 hadi 0 pamoja na kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka 5 kwa mwaka 2025 na hili linawezekana endapo elimu itawafikia walengwa kwa wakati.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Ndewirwa Mbise ameshiriki kikao hicho ameshauri kuwa Viongozi wa Dini na Wazee wa Mila washirikishwe katika vikao vya Afya ya Msingi ili waweze kusaidia kutoa elimu katika maeneo yao ili kina mama Wajawazito wapate elimu ya kuhudhuria Kliniki.
Pia, katika eneo la usafi wa Mazingira, Ndugu Mbise ameshauri kuwa wataalamu wafuatilie na kuhakikisha vikao vya vijiji na Kamati mbalimbali hasa Kamati ya Mazingira zikae ili kujadili masuala ya Mazingira.
Mhe. Mkalipa amesisitizia wataalamu kusimamia kwa karibu huduma zinazotolewa na mfuko wa Afya ya Jamii iliyoboreshwa (iCHF) ili wananchi kuona faida ya kujiunga na mfuko huo.