Waheshimiwa Madiwani ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango wamefanya ukaguzi wa mradi wa TASAF wa ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike katika Sekondari ya Malula iliyopo Kijiji cha Nrumangeny Kata ya Malula uliotengewa fedha sh. Milioni 168,042,406.22.
Ujenzi wa Mradi huo ulianza tarehe 29, Mei 2024 kwa nguvu za wananchi ambapo walichimba msingi, kuweka mawe na kujaza kifusi kwa kiasi cha shilingi Milioni 10.6 na hadi sasa mradi huo umetumia fedha sh. Milioni 18.5 ukiwa hatua ya kufungwa Lenta.
Aidha, mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 29, Septemba 2024 ili kuweza kufanya maandalizi ya kupokea wanafunzi kwa mwaka 2025.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Malula Mwl. Rehema Mrosso ameishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani mradi huu utasaidia kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu lakini kuepuka Mimba kwa wanafunzi pamoja na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi kwani watapata utulivu katika kusoma.
Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango wametoa pongezi kwa kamati ya ujenzi wa bweni hilo kwa usimamizi mzuri na kusisitiza kuendelea kufanya ukaguzi wa kila hatua ya ujenzi inayofanyika ili mradi huo ujengwe kwa ubora unaotakiwa.
Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Malula Mhe. Lukumbwe Ndossi ameiomba Serikali iendelee kusaidia katika ujenzi wa mabweni ya wavulana kwani watoto wa kiume nao wanapitia changamoto nyingi na wanahitaji kulindwa sana kwani utandawazi umeharibu maadili ya kitanzania.
Ukaguzi huo ni utaratibu wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha robo ya nne kwa mwaka wa Fedha 2023/2024.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa