Wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru wakumbushwa kuuza mazao yao bila kuzidisha kipimo kinachotakiwa ili uuzaji huo kuwa na tija na manufaa zaidi .
Akizungumza na mwandishi wetu ,Afisa kilimo Digna Masawe amesema Serikali ilishapiga marufuku uuzaji wa mazao kwa kiasi kilichozidi maarufu kama rumbesa ili Kilimo kuwa na tija kwa mkulima .
Digna amehimiza ni muhimu kwa wakulima kuwa mstari wa mbele kupinga rumbesa kwa kuungana na kuuza mazao kwa kipimo kinachotakiwa sambamba na kutoa taarifa za wanaoendeleza uuzaji wa rumbesa, "Serikali imeshazuia uuzaji wa mazao kwa rumbesa. Ni wajibu wa mkulima na mnunuzi kufuata maelekezo hayo "amesisitiza Digna
Pia, Digna amesema katika Halmashauri ya Meru kuna vikundi na umoja wa Wakulima ambapo ametoa wito kwa Wakulima kujiunga kwenye umoja wa Wakulima unaojihusisha na uuzaji wa mazao ya Wakulima (Amcos) ili waweze kuuza mazao yao kwa kilo ambapo amesema umoja wa Wakulima katika Kata ya Mbuguni Muvikiho umeweza kudhibiti Rumbesa kwani kwa sasa Wakulima wa umoja huo wanauza mazao yao kwa kilo.
Digna amesema Mkulima ana nafasi Kubwa kudhibiti Rumbesa ambapo amesema Ngarenanyuki ni miongoni mwa Kata zenye vikundi vya Wakulima ambao wanapaswa kuwa wamoja kupinga uuzaji kwa kipimo kilichozidi (Rumbesa), " Juma lililopita wataalam wa kilimo tulikuwa katika Kata ya Ngarenanyuki kutoa elimu juu ya maswala ya kilimo ikiwemo kipimo Cha uuzaji mazao ambapo tuliwakumbusha Wananchi kuepuka uuzaji wa mazao kwa kipimo kilichozidi ,hivyo nitoe Wito kwa Wananchi wa Ngarenanyuki kujiunga na Amcos ya Uwano Moja" amesema Digna
Ikumbukwe baada ya Serikali kupiga marufuku uuzaji wa Rumbesa Halmashauri ya Wilaya ya Meru ilishatoa elimu ya udhibiti wa ufungaji mazao kwa kipimo kilichozidi pamoja na kuwaelekeza Viongozi wa ngazi za Kata na Vijiji kudhibiti Rumbesa kwenye maeneo yao.
Pia. Halmashauri Kupitia mawakala inakusanya tozo za mazao kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali kuhusiana na kipimo.
Aidha,Halmashauri inatoa wito kwa Wakulima na Wananchi kwa ujumla kutoa taarifa kwa Wataalamu wa kilimo Ngazi za Kata, Uongozi wa Kata, Vijiji na Wilaya juu ya wanunuzi wa mazao na wakulima ambao bado wanaendeleza uuzaji wa mazao kwa kipimo kilichozidi maarufu kama rumbesa inayolenga kumkandamiza mkulima
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa