Halmashauri ya Wilaya ya Meru kupitia idara ya elimu msingi imetoa motisha kwa Walimu, Wanafunzi, Shule na Kata zilizofanya vizuri katika mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2021.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya utoaji motisha, Mkuu wa Idara ya elimu ya awali na msingi Mwl. Marcus Nazi amesema motisha hiyo ni hamasa kwa walimu,uongozi wa shule na jamii kushiriki kikamilifu kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata elimu bora ambapo kwa shule zilizofanya vibaya zimepewa cheti cha onyo ili kuwakumbusha uwajibikaji. "tunatambua mchango wa walimu , kazi mnayofanya ni kubwa na sisi tupo nyuma yenu.”Amesema Mwl.Nazi
Mwl.Nazi amesema elimu ya msingi ni muhimu kwani mtihani wa kumaliza elimu ya msingi unapima kiwango cha kumudu stadi na maarifa aliyoyapata mwanafunzi kwa miaka 7 hivyo ufundishaji na usimamizi mzuri huchangia kwa kiasi kikubwa kumwezesha mwanafunzi kufanya vizuri .
Katibu tawala Wilaya ya Arumeru Mwl.James Mchembe ambaye amemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo , amepongeza walimu kwa ufaulu mzuri ,ambapo Halmashsuri ya Wilaya ya Meru imeshika nafasi 3 Kimkoa "niwapongeze kwa matokeo haya mazuri,nitoe wito kwenu walimu tuendelee kutekeleza majukumu kwa ufanisi mkubwa kwani Mhe.Rais wetu anawajali watumishi na ameshaanza kuboresha maslahi ya watumishi"amesema Mwl.Mchembe
Mwenyekiti wa chama cha Walimu (CWT)Wilaya ya Arumeru Isaack Kamalang'ombe amesema Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi kifupi imeleta neema na kuongeza nuru kwa walimu na watumishi wengine ambapo watumishi walinufaika na mserereko wa kupanda madaraja, kubadilishiwa muundo ,punguzo la kodi ,kupandisha asilimia ya kikokoto cha pensheni sambamba na maboresho mengine yaliyoridhiwa na yanayotarajiwa kuanza mwaka wa fedha ujao "hakuna haki bila wajibu ,wito wangu kwenu tuendelee kutekeleza wajibu wetu"amesema kalamang'ombe.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Walimu wa shule na masomo yaliyofanya vizuri wameishukuru Halmashauri kwa kutambua mchango wao na kutoa wito kwa shule zilizo fanya vibaya kuongeza juhudi kupandisha ufaulu "tunashukuru kwa motisha hii,tunaahidi kufanya vizuri zaidi "amesema Tajieli Mbwambo ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Leganga ambayo ni miongoni mwa shule zilizopandisha ufaulu.
Dkt.Amani Sanga ambaye amwemwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru amewashukuru wadau na wote waliohusika kufanikisha hafla hiyo inayolenga kuchochea kupanda kiwango cha ufaulu Meru.
Mhe, Kaanael Ayo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu ,Afya na Maji amekabidhi vyeti vya pongezi na fedha taslimu kiasi cha shilingi laki moja kila mmoja kwa walimu 12 waliofaulisha zaidi katika masomo yao, madaftari/ counter books 5, Rimu moja ya karatasi na cheti cha pongezi kwa wanafunzi 4 waliofanya vizuri wakiwemo wa elimu maalum. Amekabidhi vyeti vya pongezi na Sukari kwa makundi ya shule bora 10 za serikali na zisizo za serikaali zilizokuwa na watahiniwa zaidi 40,shule bora 10 za serikali na zisizo za Serikali zilizokuwa na watahiniwa chini ya 40,shule 10bora za serikali zilizokuwana watahiniwa zaidi 40 na shule bora 10 za serikali zilizokuwa na watahiniwa chini 40 .Katika kila kundi shule ya kwanza imepewa kg 25 za sukari shule ya 2-3 kg 20 na Shule ya 4 hadi ya 10 zimepewa sukuri kg 10.
Pia Mhe.Ayo amekabidhi vyeti vya pongezi kwa Shule 10 zilizopandisha ufaulu, cheti cha pongezi kwa Kata tatu zilizopandisha ufaulu,cheti cha onyo kwa shule 10 zilizoshuka ufaulu, cheti cha onyo kwa kundila shule 5 zilizokuwa na watainiwa zaidi ya 40 na zilizokuwa na watainiwa chini 40,cheti cha onyo kwa Kata 3 zilizoshuka ufaulu na cheti kwa Mdau wa The foundationi for tommorow.
Halfla ya utoaji motisha imefanyika katika ukumbi wa Shule ya Msingi Mariado
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa