WANAWAKE TUWARITHISHE WATOTO WETU MAARIFA - DC KAGANDA.
Imewekwa: March 8th, 2024
Siku ya Wanawake Duniani 08.03.2024
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Kaganda kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John VK. Mongella, ambaye ni mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Ngarenaro Mkoa wa Arusha, amesema kuwa wanawake wote wajifunze kuwarithisha watoto wao vipaji mbalimbali na shughuli wanazozifanya ili ziweze kuwasaidia watakapokuwa wakubwa.
Amesema hayo baada ya kutembelea mabanda mbalimbali na kukuta watoto katika banda la Halmashauri ya Wilaya ya Meru wakitengeneza bidhaa mbalimbali za urembo na kuuza wakiwa pamoja na wazazi wao.
"Nimefurahishwa sana na watoto wadogo walianza kujifunza ujasiriamali mapema kwani hii itawasaidia kuwa wabunifu na kujipatia kipato ambapo wataweza kutatua changamoto zao" Alisema Kaganda.
Aidha, Mhe. Kaganda amewataka wanawake kujiamini na kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwani mwanamke ana ushawishi katika chachu ya kuleta maendeleo kwa jamii.
Hata hivyo, Mhe. Kaganda ametoa rai kwa wanawake wote wanaoishi kwenye mahusiano ambayo hayana maelewano kuwa waachane na mahusiano hayo hasa yale yanayopelekea kuhatarisha maisha.
Kaganda ametumia muda huo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mwanamke jasiri na shupavu aliyeweza kuiongoza Nchi ya Tanzania kwa Amani na Utulivu wa hali ya juu ikiwa ni pamoja na kuleta maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali hapa nchini.
Kauli Mbiu ya mwaka 2024 "Wekeza kwa Mwanawake ili Kuharakisha Maendeleo ya Taifa Pamoja na Ustawi wa Jamii"