Na Annamaria Makweba
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA Wilaya ya Arumeru imefanikiwa kuandikisha wananchi 393,275 sawa na asilimia 98 ya lengo la uandikishaji.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Kaganga akizindua rasmi zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa wakazi wa Wilaya ya Arumeru.
Mhe. Kaganda amefanya uzinduzi huo katika Viwanja vya Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Meru ambapo wananchi na viongozi mbalimbali wameshiriki katika Uzinduzi huo.Kaganda ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa maelekezo ya kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na Kitambulisho chenye taarifa sahihi za Uraia halisi wa mtu husika zinazoweza kutumika kumtambilisha mahali popote.
Aidha, Kaganda ametoa rai kwa jamii kuwa waaminifu wakati zoezi la ugawaji wa vitambulisho unafanyika na kutofanya vitendo vya kuhujumu zoezi hilo. Vilevile ameitaka jamii kuhamasisha Watanzania wote waliofikisha umri wa miaka 18 kufika ofisi za NIDA ili waweze kujiandikisha, kusajiliwa na kupata vitambulisho. Kaimu Afisa Usajili Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA Arumeru, Soud S. Kibanga ameeleza changamoto kubwa katika zoezi la ugawaji wa vitambulisho ni wananchi kutofika kwa wakati kuchukua vitambulisho vyao na wengine kubadili majina au kutokumbuka taarifa zao. Christina Kenje Mao na wananchi wengine walioshiriki katika zoezi hilo wamepatiwa Vitambulisho vya Taifa vilivyotolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo katika uzinduzi uliofanywa tarehe 6.12.2023.
Mheshimiwa Diwani Kata ya Songoro, Kaanael Ayo ametoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuisimamia vyema Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ilianzishwa mwaka 2008 kwa tangazo la Gazeti la Serikali GN No. 122 kama chombo cha kusimamia utoaji wa vitambulisho vya Taifa, na Wilayani Arumeru zoezi lilianza rasmi mwaka 2016 kwa kuanza na watumishi wa Serikali na baadaye wananchi wengine.