WILAYANI ARUMERU WAPOKEA KWA SHANGWE UJIO WA SAFARI ZA TRENI BAADA YA MIAKA 30 .
Wenyeviti wa Vijiji na Viongozi Wilayani Arumeru wameishukuru Serikali Kwa kuhakikisha mwananchi wa hali ya chini anaweza kusafiri kwa gharama nafuu na salama zaidi kwa Kurejesha safari za Reli Mkoani Arusha
Hayo yamejiri wakati wa ufunguzi rasmi wa kampeni ya uelewa kuhusu usalama katika njia ya reli na ulinzi wa miundombinu ya reli ambayo imeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Idd Kimanta Wilayani humu ambapo imewakutanisha Maafisa Tarafa, Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji, Watendaji wa Kata na Vijij vinavyopitiwa na Reli , Uongozi wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri ya Meru na Arusha pamoja na maafisa toka shirika la reli hapa Nchini (TRC).
Mhe.Kimanta amesema Serikali imekusudia safari za treni katika Mkoa wa Arusha kuanza hivi karibuni (mwishoni mwa mwezi Agosti) ambapo wananchi wa Mkoa huo watapata fursa ya kusafiri na kusafirisha mizigo kwa gharama nafuu ikilinganishwa na gharama za usafiri mwingine.
Mkuu wa Kitengo cha habari na uhusiano wa Shirika la Reli nchini Bi Jamila Mbaroukamesema usafiri wa treni ni usafiri salama zaidi na wa gharama nafuu hivyo Viongozi na wananchi hawana budi kuunga mkono juhudi za Serikali za kurejesha safari za Reli Mkoani Arusha ambazo zilisimama kwa zaidi ya Miaka 30.
Maizo Mgedzi, Mkuu wa Kitengo cha udhibiti wa ajali katika njia ya reli TRC ametoa wito kwa Viongozi wa Vijiji na Vitongoji vinavyopitiwa na reli kuwakumbusha na kuwajulisha wananchi hasa walio karibu na reli ujio wa safari za Treni Mkoani Arusha Mwezi huu ili waweze kuwa salama na kunufaika na usafiri huo wa gharama nafuu.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Ndg.Jerry Muro kwa niaba ya Wananchi wa Wilaya hiyo amemshukuru Mheshimiwa Rais kwani urejeshaji wa safari hizo mkombozi kwa watanzania na kuahidi kuitunza, kuilinda na kuitumia reli hii.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa