Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango ametoa wito kwa viongozi wa dini, viongozi wa mila, wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji ,Waheshimiwa Madiwani na Watendaji wa Serikali kuhamasisha jamii kushiriki zoezi la sensa ili Kupata takwimu za msingi zitakazosaidia kuainisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi maalum yenye uhitaji maalum kwa mfano, watu wenye ulemavu, wanawake, watoto, vijana na wazee hivyo kurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na uhitaji na mazingira yaliyopo.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na viongozi wa Tarafa ya Poli na King'ori Mhe.Ruyango amesema tarehe 23 Agosti 2022 kila Mtanzania aliyelala ndani ya Wilaya hiyo awe Mkazi au la anapaswa kuhesabiwa ambapo amehimiza viongozi kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi kutoa ushirikiano kufanikisha zoezi la sensa ya watu na makazi " nitoe wito kwenu viongozi mkawe wazalendo kwani Tanzania inajengwa na watanzania hivyo tushirikiane kuhakikisha zoezi la sensa linafanikiwa katika maeneo yetu" amehimiza Mhe.Ruyango.
Daudi Wengi ambani ni Afisa Mipango wa Halmashauri ya wilaya ya Meru akimwakilisha mratibu wa Sensa amefafanua kuwa tarehe 23 Agosti 2022 itabaki kuwa tarehe rejea ya Sensa ambapo watu wote waliyolala usiku wa kuamkia tarehe 23 watahesabiwa ambapo ametoa wito kwa wakuu wa kaya kuwa na taarifa zote muhimu za watu waliolala kwenye kaya yake usiku wa kuamkia tarehe ya sensa ambapo amebainisha taarifa hizo ni umri, jinsi,hali ya ndoa,elimu ,shughuli za kiuchumi ,umiliki wa vitambulisho vya taifa nk
Kwa upande wao Viongozi wa Dini na Mila waliohudhuria mkutano wa uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi wametoa wito kwa jamii kushiriki zoezi la Sensa ili kutoa taarifa sahihi ili kuwezesha Serikali kutimiza wajibu wake kwa wananchi kulingana na idadi ya watu ya eneo husika " nitoe wito kwa wananchi kushiriki kuhesabiwa katika zoezi la sensa pia sisi kama viongozi wa mila hatutaruhusu mtu yeyote kuleta Mgogoro kwenye zoezi la Sensa" amesema Hezron Sumary Mshili Mkuu Meru
Naye Ramadhan Omary Sheik Wa Usa-River na Amani Halisi Kuhani wamesema kama viongozi wa dini watahakikisha jamii inaendelea kuhamasika na kushiriki katika zoezi la Sensa kwa maendeleo ya nchi.
Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji pamoja na viongozi wengine wa Halmashauri hiyo wakiongozwa na Mhe.Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki wametoa wito kwa wananchi kujitokeza kuhesabiwa kwa kutoa taarifa sahihi zitakazotumika kuwaletea maendeleo
Aidha vikao vya kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika zoezi la Sensa Vimefanyika katika Tarafa tatu za Halmashauri ya Wilaya ya Meru na kuwa jumuisha viongozi wa Dini ,Mila ,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji ,Waheshimiwa Madiwani ,Watendaji wa kata na Vijiji vyote vya Halmashauri ya Wilaya ya Meru .
SENSA KWA MAENDELEO JIANDAE KUHESABIWA
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa